Iran yalaani jinai na uvamizi wa mfululizo wa Israel dhidi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119960-iran_yalaani_jinai_na_uvamizi_wa_mfululizo_wa_israel_dhidi_ya_syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali uvamizi na mashambulizi ya mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni dhidi ya miundombinu ya Syria ambapo Israel imeteka na kukalia kwa mabavu maeneo mengine ya Syria katika kipindi cha siku chache zilizopita.
(last modified 2024-12-10T03:03:58+00:00 )
Dec 10, 2024 03:03 UTC
  • Iran yalaani jinai na uvamizi wa mfululizo wa Israel dhidi ya Syria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali uvamizi na mashambulizi ya mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni dhidi ya miundombinu ya Syria ambapo Israel imeteka na kukalia kwa mabavu maeneo mengine ya Syria katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Katika matamshi yake ya kulaani jinai zisizo na kikomo za utawala katili wa Israel, Ismail Baqaei amezilalamikia vikali nchi za Magharibi kwa uungaji mkono wao kwa jinai na uvamizi wa Israel.

Amegusia pia jinsi utawala wa Kizayuni ulivyovamia na kuteka maeneo zaidi ya Syria wakati huu ambapo kuna ombwe la kiutawala nchini humo baada ya kupinduliwa serikali ya Rais Bashar al Assad na kusema kuwa, jinai hizo za Israel ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo lichukuke hatua za haraka za kukomesha jinai hizo za utawala wa Kizayuni.

Amekumbushia pia suala la milima ya Golan ya Syria na jinsi utawala wa Kizayuni ulivyoteka na kukalia kwa mabavu maeneo zaidi ya milima hiyo katika siku chache zilizopita akisema kuwa, huo ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesema, utawala wa Kizayuni unaendelea kuonesha dhati yake ya kutoheshimu sheria zozote za kimataifa.

Ikumbukwe kuwa, kuanzia tarehe 27 Novemba 2024, na kwa uungaji mkono wa baadhi ya nchi, magaidi na wapinzani wenye silaha nchini Syria walifanya mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Syria katika maeneo tofauti ya nchi hiyo, na hatimaye yalipelekea kuanguka serikali ya Syria siku ya Jumapili ya Disemba 8, 2024.