Ubalozi wa Iran nchini Syria kufunguliwa hivi karibuni
Hossein Akbari Balozi wa Iran nchini Syria ameeleza kuwa ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu mjini Damascus ambao ulifungwa kufuatia matukio ya karibuni katika nchi hiyo ya Kiarabu utaanza shughuli zake hivi karibuni.
"Lengo letu ni kurejesha shughuli za ubalozi haraka iwezekanavyo. Watu hawa (makundi yanayoidhibiti Syria) wameelezea utayarifu wao wa kudhamini usalama kwa ajili ya ubalozi huo na shughuli zake", amesema Balozi wa Iran nchini Syria katika mahojiano na kanali ya habari ya hapa nchini jana usiku.
Balozi Hossein Akbari ameongeza kuwa vifaa na wafanyakazi wa ubalozi huo wamehamishiwa Beirut, Lebanon kwa siku mbili tatu ili kuwadhaminia usalama wao na kuepusha uharibifu wowote unaoweza kutokea, lakini inshallah ubalozi wa Iran utaanza kazi zake hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo, Balozi wa Iran nchini Syria ametupilia mbali dhana kuwa Syria inaweza kuwa Libya ijayo, akisema kuwa nchi hizo mbili zina hali tofauti za kijiografia na mazingira ya kikanda.