Safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran mjini Kabul
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amefanya safari yake ya kwanza rasmi mjini Kabul tangu wanamgambo wa Taliban waliporejea tena madarakani nchini Afghanistan Agosti 2021.
Katika safari yake hiyo siku ya Jumapili, Araghchi alikutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Kabul kuhusu masuala muhimu yakiwemo haki ya maji ya Iran, usalama wa mipaka na ushirikiano wa pande mbili.
Safari hiyo imelenga kuimarisha uhusiano wa Iran na Afghanistan na kukabiliana na changamoto za pamoja kama vile uhamiaji, madawa ya kulevya na usalama wa mipaka. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, mazungumzo na mashauriano ya Tehran na Kabul yanaweza kusaidia kupunguza mivutano ya kikanda na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi.
Safari ya Araghchi mjini Kabul imefanyika katika hali ambayo, Afghanistan inakabiliwa na changamoto za kiusalama na kiuchumi, na Iran inataka kuimarisha uhusiano wake na nchi jirani hususan katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Akiwa nchini Afghanistan, Abbas Araghi alikutana na kubadilishana mawazo na viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Taliban akiwemo Waziri Mkuu, Hassan Akhund, Kaimu wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni Mawlawi Amir Khan Muttaqi na Waziri wa Ulinzi Muhammad Yaaqob.
Moja ya mambo aliyoyatilia mkazo Abbas Araghchi katika mazungumzo na mashauriano yake na watawala wa serikali ya muda ya Afghanistan ni haki ya Iran ya maji katika mto Helmand.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Mapatano ya Helmand yaliyosainiwa Februari 20 mwaka 1973 yameainisha wazi haki ya Iran ya kustafidi na sehemu yake ya maji ya mto huo.
Hata hivyo kutokana na kuathiriwa na mashinikizo na chokochoko za ndani na nje, serikali mbalimbali za Afghanistan zimekwepa kutekeleza wajibu wao wa kudhamini haki hiyo ya Iran.
Mto Helmand, wenye urefu wa kilometa 1,126, unaanzia kutoka milima ya Hindu Kush nchini Afghanistan na kuelekea Iran. Mamilioni ya wananchi kutoka pande mbili hizi hutegemea sana maji kutoka mto huo katika umwagiliaji, uvuvi, na matumizi mengine ya nyumbani.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Afghanistan inatakiwa kila mwaka iruhusu maji angalau mita za ujazo milioni 850 zitiririke hadi Iran, “katika hali ya kawaida.
”Kwa miongo minne sasa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mwenyeji wa moja kati ya idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani hasa raia wa Afghanistan. Hata katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran na pia pamoja na kuwepo vikwazo vya kidhalimu vya miongoni minne, Iran imeendelea kutoa huduma kwa mamilioni ya wakimbizi Waafghani ambao wanafanya kazi, kusoma na kuishi nchini bila vizingiti.
Baada ya kuingia madarakani utawala wa Taliban nchini Afghanistan, idadi kubwa ya Waafghani walikimbia nchi yao kuelekea Iran. Pamoja na kuwepo matatizo ya kiuchumi yatokanayo na vikwazo vya kidhalimu na pasina kuwepo misaada ya kimataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewapokea kwa mikono miwili wakimbizi kutoka Afghanistan.Afghanistan iko katika hali mbaya ya kiuchumi kwa namna ambayo hivi karibuni duru za kimataifa zimesema uchumi wa nchi hiyo unakaribia kusambaratika. Hii ina maana kwamba uchumi huo unahitajia kuboreshwa na kuimarishwa haraka kwa msaada wa nchi za eneo.
Ni jambo lisilo na shaka kuwa, kuimarishwa kwa uhusiano wa pande mbili kutakuwa na maslahi kwa pande zote mbili. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Abbas Araghi akasisitiza katika mazungumzo yake na viongozi wa Taliban juu ya udharura wa kufunguliwa ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Tehran na Kabul jambo ambalo limepokewa pia kwa mikono miwili na viongozi wa Taliban.