Sudani Kusini: Serikali yawasilisha mpango kazi wa kutekeleza makubaliano ya amani
Nchini Sudani Kusini, wakati mzozo wa kisiasa na kijeshi ukiendelea, serikali ya nchi hiyo imewasilisha mpango kazi wenye lengo la kutekeleza makubaliano ya amani.
Ripoti zinasema, serikali ya Juba inajaribu kuwahakikishia raia kuhusu mustakabali wa makubaliano ya amani. Siku ya Jumamosi, Aprili 26, Waziri wa Masuala ya Baraza la Mawaziri, Martin Elia Lomuro aliwasilisha mpango kazi wa kutekeleza makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka wa 2018, ambayo yalipelekea kuundwa kwa serikali ya umoja na ya mpito.
Mnamo Machi 26 mwaka huu, Makamu wa Rais, Riek Machar, aliwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani na Rais Salva Kiir, kwa sababu alituhumiwa kuandaa vurugu dhidi ya jeshi la Sudani Kusini huko Nasir (NASSIR), kaskazini mashariki mwa nchi.

Utekelezaji wa makubaliano ya amani ya 2018 umekuwa wa polepole, huku hali ya taharuki ikiongezeka kufuatia mapigano ya hivi karibuni kati ya kikundi cha waasi kinachojiita White Army, kinachoaminika kuwa na uhusiano na Machar.
Mivutano na hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kati ya pande mbili za Kiir na Machar na ilishtadi mnamo mwezi Februari wakati kundi liitwalo Jeshi Jeupe, lilipovamia kambi ya jeshi katika jimbo la Upper Nile na kushambulia pia helikopta ya Umoja wa Mataifa.