Wapalestina wengine 51 wauawa shahidi katika hujuma ya kinyama ya Israel
(last modified Sun, 27 Apr 2025 12:35:26 GMT )
Apr 27, 2025 12:35 UTC
  • Wapalestina wengine 51 wauawa shahidi katika hujuma ya kinyama ya Israel

Kwa akali Wapalaestina 50 wameuawa shahidi katika mashambulio ya kinyama ya karibuni zaidi kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza huku idadi ya vifo ikiendelea kuongezeka.

Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa watu 51 wameuawa na wengine 115 wamejeruhiwa huko Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita.

Wakati huohuo Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa hadi sasa watu 1,978 wameuawa shahidi na wengine 5,207 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni ulipovunja makubaliano ya usitishaji mapigano mnamo Machi 18, 2025.

Wapalestina wapatao 52,243 wamethibitishwa kuwa wameuawa shahidi na wengine 117,248 wamejeruhiwa katika vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza Oktoba 7, 2023.

 

Katika upande mwingine ripoti mbalimbali zinasema kuwa, hali ya kibinadamu huko Gaza ni mbaya sana. Umoja wa Mataifa umesema kuwa umekumbwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kutahadharisha kuwa eneo hilo linapitia katika hali ngumu sana tangu kuanza vita dhidi ya ukanda huo.

Utawala wa Kizayuni tangu tarehe 18 Machi mwaka huu baada ya kukiuka makubaliano ya usitishaji vita,  si tu kuwa umefunga njia za kugawa misaada na kuingiza bidhaa za chakula na dawa katika Ukanda wa Gaza lakini pia Israel umefanya mashambulizi makubwa ya anga katika maeneo mbalimbali ya Gaza, ikiwa ni pamoja na kuzishambulia na mahema ya wakazi wa Gaza, jambo ambalo limesababisha kuongezeka kwa idadi ya vifo vya raia wa Kipalestina.