OIC yalaani hatua ya Marekani dhidi ya shirika la UNRWA
(last modified Sun, 27 Apr 2025 12:11:37 GMT )
Apr 27, 2025 12:11 UTC
  • OIC yalaani hatua ya Marekani dhidi ya shirika la UNRWA

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imelaani vikali uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuliondolea kinga ya kisheria Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Wapalestina (UNRWA).

Taarifa ya OIC imesema, imesikitishwa na hatua ya Marekani ya kuliondolea kinga ya kisheria Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Wapalestina UNRWA na kuitaka Washington iuangaalie upya uamuzi wake huo na kurejesha ufadhili wake wa kifedha kwa shirika hilo.

Jumuiya ya OIC imetoa taarifa na kutangaza kuwa, UNRWA haiwezi kuwa kitu kisichohitajika kuwepo au nafasi yake kuchukuliwa na taasisi nyingine; na kwamba taasisi hiyo ni mshipa wa uhai wa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina hususan katika Ukanda wa Ghaza.

Siku ya Ijumaa ya tarehe 25 Aprili, serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump iliamua kufuta kinga liliyokuwa nayo shirika la utoaji misaada la UNRWA. Kwa uamuzi huo, serikali ya Marekani haitaitambua tena UNRWA kuwa ni sehemu ya mashirika ya Umoja wa Mataifa, jambo ambalo litatoa ruhusa ya shirika hilo kushtakiwa katika mahakama za nchi hiyo.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutoa Misaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu, kwa kifupi UNRWA, ni shirika la Umoja wa Mataifa lililoanzishwa mwaka 1949.

UNRWA ina jukumu la kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Kipalestina ambao wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano ya muda mrefu. Kwa maneno mengine ni kuwa, shirika hili linatoa huduma za kijamii, elimu, afya na misaada mingineyo kwa wakimbizi wa Kipalestina ambao wamehamishwa kwa nguvu katika maeneo yao kutokana na vita, machafuko na utumiaji nguvu.