Mkutano wa 3 wa Kiuchumi wa Iran na Afrika umeanza mjini Tehran
Mkutano wa 3 wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika umeanza leo hapa Tehran na utaendelea hadi tarehe 29 mwezi huu wa Aprili. Mkutano huu aidha utaendelea katika mji wa Isfahan hapa nchini tarehe 29 hadi 30 Aprili.
Mkutano wa 3 wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika unaangazia maeneo makuu manne: Mafuta- gesi- petrokemikali, sekta ya madini, kilimo na nishati.
Mkutano wa tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika unafanyika kwa wakati mmoja na Maonyesho ya Iran ya Expo 2025. Mkutano huu umetajwa kuwa fursa kwa wageni kutoka Afrika ili kufahamu uwezo na suhula za Iran ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazouzwa na nchi hii katika nchi mbalimbali duniani.
Bara la Afrika, lenye jamii inayoongezeka na rasilimali tajiri, ni soko kubwa la bidhaa mbalimbali. Kwa kuzingatia ongezeko kubwa la mabadilishano ya kibiashara na bara la Afrika, wafanyabiashara wa Iran kwa sasa wanahitaji mipango makini na uwekezaji thabiti ili kuwa na ushiriki mkubwa katika masoko ya nchi za Kiafrika.
Biashara kati ya Iran na nchi za Afrika imekua kwa asilimia 10.5 na kuwa na thamani ya asilimia 39 tangu mwaka 2022. Wakati huo huo, Iran na Afrika zinataraji kuwa na mabadilishano ya kibiashara yenye thamani ya dola bilioni 10 mwaka huu wa 2025.