Imam Khamenei: Gaza imezipiga mweleka Marekani na Israel kwa Neema za Allah
Kiongozi Muadhami wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hakuna mtu yeyote angelifikiria mwaka jana kwamba, Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wangeliibuka washindi dhidi ya muungano wa Marekani na Israel.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili katika kikao na washiriki wa Duru ya 41 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran na kuongeza kuwa, "Gaza itaibuka mshindi mkabala wa utawala wa Kizayuni."
Kiongozi Muadhamu amehoji, "Iwapo ungeliambiwa kwamba eneo dogo kama Gaza litalazimika kukabiliana dhidi ya dola kubwa lenye nguvu za kijeshi kama Marekani, na wangepambana vilivyo, na Gaza iibuke mshinde, je, kuna mtu yeyote angeliweza kuamini? Lakini kwa Neema ya Allah, imewezekana.”
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ndiyo nchi pekee duniani inayozungumza dhidi ya Marekani na kuitaja kwa majina yake halisi.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, "Tofauti kati ya taifa la Iran na mataifa mengine ni kwamba [Iran] ina ujasiri wa kusema ukweli huu kwamba Marekani ni mchokozi, mwongo, mdanganyifu na mkoloni na haifuati kanuni na sheria zozote za kibinadamu."
Amesema, “Taifa la Iran limeonyesha subira na ustahimilivu kwa zaidi ya miaka 40, huku madola yote ya kiistikbari yakisimama na kupanga njama dhidi yake." Imam Khamenei amebainisha kuwa, "Sio tu kwamba taifa la Iran halijadhurika, lakini pia limepiga hatua za maendeleo na kustawi. Iran ya leo, sio Iran ya miaka 40 iliyopita, tumepiga hatua katika kila nyanja."
Kwingineko katika hotuba yake kwenye mkutano wake na washiriki wa Duru ya 41 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran, Kiongozi Muadhamu amehimiza kuikimbilia Qur'an Tukufu kwa ajili ya kutatua matatizo. Ameeleza bayana kuwa, "Kila kitu ndani ya Quran ni muujiza. Tukiitumia Qur'an (ipasavyo), matatizo yote yatatatuliwa."
