IRGC: Tutazindua karibuni kombora la 'supersonic cruise'
Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu karibuni hivi itazindua kombora la kisasa la cruise lenye uwezo wa kusafiri kwa mwendo kasi wa supersonic, lililotengenezwa na wataalamu wa humu nchini.
Admeli Alireza Tangsiri alisema hayo akielezea maendeleo ya hivi karibuni katika nguvu ya majini ya nchi na kuongeza kuwa, kombora hilo jipya, ambalo litazinduliwa katika mwaka ujao wa kalenda ya Kiirani (utakaoanza Machi 20) litaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa wa Iran wa kujihami na kuzuia hujuma.
Habari zaidi zinasema kuwa, kombora hilo la supersonic lina uwezo wa kupiga shabaha umbali wa kilomita 2,000 (maili 1,242) kwa usahihi, na hivyo kuimarisha uwezo wa juu wa kijeshi wa nchi hiyi katika ulinzi wa majini.
Admeli Tangsiri ameeleza bayana kuwa, "Sasa tuna makombora ambayo yanaweza kurushwa kutoka ndani kabisa ya ardhi ya Iran, na kuondoa hitaji la kuyarusha tokea pwani."
Kamanda huyo wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la SEPAH amefafanua kwa kusema, "Kwa ustawi huu, tunaweza kulenga shabaha katika Bahari ya Oman moja kwa moja kutoka kaskazini [sehemu] ya Ghuba ya Uajemi."

Wataalamu na wahandisi wa kijeshi wa Iran katika miaka ya hivi karibuni wamepata mafanikio makubwa katika utengenezaji wa aina mbalimbali wa zana za kivita ndani ya nchi, na hivyo kuvitosheleza vikosi vyake vya kijeshi na kuvifanya visitigemee msaada wa kigeni.
Viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba, nchi hii haitasita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na uwezo wa makombora kwa ajili ya kujilinda dhidi ya adui, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitafungua mlango wa majadiliano na yeyote yule kuhusu suala hilo.