Iran: Tunapinga mpango wowote wa kufukuzwa Wapalestina Gaza
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Bagher Ghalibaf amesema kuwa Tehran inapinga vikali na kulaani mpango wowote unaokusudia kuwafurusha Wapalestina katika ardhi zao.
Akihutubia Kikao cha 15 cha Bunge la Asia (APA) leo Jumatano, Ghalibaf amekosoa matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu Gaza, akiyataja kuwa hayana msingi, ni ya kibeberu, na yamefichua malengo ya kikoloni ya Marekani huko Palestina.
Ghalibaf ameeleza bayana kuwa, mpango wa kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu unathibitisha zaidi Marekani na Israeli haziheshimu hata kidogo haki za binadamu.
Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, kile kinachoitwa "mpango wa amani" wa Trump, ambao ulipendekezwa katika muhula wake wa kwanza wa uongozi, si chochote ila ni mfumo wa kisasa wa ubaguzi wa rangi; na ni mradi wa kuhudumia maslahi haramu ya Israel kwa kufuta utambulisho wa Wapalestina na kukandamiza matakwa yao ya kujitawala.

"Iran inapinga suluhisho lolote ambalo linapuuza matakwa ya watu wa Palestina na kuongeza kuwa, mpango huo wa Trump ni tishio la moja kwa moja kwa usalama na uthabiti wa kikanda," amesisitiza Ghalibaf.
Ameongeza kuwa, mustakabali wa Palestina hautaamuliwa na Marekani au mamlaka yoyote ya kikoloni; na kwamba ni lazima uamuliwe tu na watu wa Palestina kwa njia ya haki na ya kidemokrasia.
Ametoa wito kwa nchi zote huru na mashirika ya kimataifa hususan mabunge ya Asia kuchukua msimamo thabiti dhidi ya njama hizo mpya na kuwaunga mkono kikamilifu Wapalestina kwa kauli na vitendo.