Siku ya Wanawake; Iran yataka Israel itimuliwe UN + Picha
Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imetaka utawala wa Kizayuni utimuliwe kutoka kwenye umoja huo kutokana na jinai kubwa unazofanya dhidi ya wananchi wa kawaida wa Palestina hasa wanawake na watoto wadogo.
Mwandishi wa Shirika la Habari la IRIB amenukuu taarifa ya ofisi hiyo ikisema kwamba, kuna wajibu wa kufukuzwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa na taasisi zake zote kutokana na jinai kubwa unazowafanyia wanawake.
Mwito huo wa Iran umetolewa baada ya Idara ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Gaza kutangaza kuwa: Wanawake 12,316 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika vita vya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Ghaza.
Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na Idara ya Habari ya Serikali ya Palestina huko Ghaza kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Wanawake imesema: "Katika vita vya Ghaza, wanawake 13,901 wamefanywa wajane na akina mama 17,000 wamepoteza watoto wao."
Taarifa hiyo imesema, wanawake na wasichana 2,000 wa Kipalestina wamepata ulemavu wa kudumu kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Israel, na katika awamu ya hivi karibuni, makumi ya wanawake wa Kipalestina wametiwa mbaroni na kuteswa ndani ya jela za Israel.
Ofisi hiyo imeeleza kuwa wanawake wa Ghaza wanakabiliwa na kifo cha polepole kutokana na kuzingirwa, ukosefu wa suhula za afya na kuzuiwa kwa misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo la Palestina. Maelfu ya wanawake wa Ghaza wamepoteza watoto wao katika mauaji ya kimbari ya Israel.
Ripoiti zinasema: Vita na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Ghaza yamekuwa na taathira kubwa zaidi kwa wanawake na watoto na hivyo kuwatengenezea mazingira magumu.
Jana tarehe 8 Machi dunia iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiendelea kupaza sauti za kulaani ukatili unaofanywa na Israel dhidi ya wanawake wa Palestina.
Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za mateso ambayo utawala katili wa Israel unawafanyia wanawake wa Palesitna.






