Iran: Kuna tofauti kati ya mazungumzo na vitisho
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema katu Jamhuri ya Kiislamu haitafanya mazungumzo kuhusu mradi wake wa nishati ya nyuklia chini ya mashinikizo, kwani mazungumzo ni tofauti na utumiaji wa mabavu na vitisho.
"Hatutafanya mazungumzo chini ya mashinikizo na vitisho. Hatutazingatia (kufanya mazungumzo), haijalishi ni mada gani (ya kujadiliwa)," Araghchi amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii X (Twitter) leo Jumatatu.
"Mazungumzo ni tofauti na uonevu na kushurutisha," ameongeza mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ambapo amesisitiza juu ya kuwa wa amani mpango wa nishati ya nyuklia wa Iran.
Araghchi amebainisha kuwa, "Kwa hivyo, kimsingi, hakuna kitu kama 'uwezekano (wa mradi wa nyuklia wa Iran kukengeuka na kuwa) wa kijeshi".
Katika ujumbe wake huo, Araghchi amesema mashauriano kati ya Iran na Troika ya Ulaya - Ufaransa, Ujerumani na Uingereza - na wakati huo huo kati yake na Russia na China kwa upande mwingine yanaendelea "kwa usawa na kuheshimiana."
Katika mahojiano na Fox News Machi 6, Rais wa Marekani, Donald Trump alidai kuwa Iran inaweza kudhibitiwa kijeshi au kwa kufanya makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Siku ya Jumamosi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema kuwa, sisitizo la baadhi ya madola ya uonevu katika kufanya mazungumzo na Iran halilengi kutatua masuala na kusisitiza kwamba Iran kamwe haitakubali matarajio ya mataifa yanayodhulumu.