Faili la nyuklia la Iran: Tehran yawaita mabalozi wa UK, Ufaransa, Ujerumani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewaita mabalozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu jaribio lao la pamoja na Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, dhidi ya mradi wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iliwaita wawakilishi hao wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani mjini Tehran jana Aklhamisi kupinga msimamo wao kuhusu mradi wa kiraia wa nyuklia wa Iran.
Wakuu wa balozi hizo za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani hapa mjini Tehran waliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran hiyo jana, ambapo Tehran imelalamikia ushirikiano wa mataifa hayo matatu ya Ulaya na Marekani katika kutumia vibaya Baraza la Usalama na kufanya kikao cha faragha kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, mabalozi wa nchi hizo waliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Tehran na Hassaninejad Pirkouhi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Amani ya Kimataifa na Usalama katika wizara hiyo.
Mabalozi wa nchi hizo tatu walisema katika mikutano hiyo kwamba watafikisha malalamiko ya Iran kwenye miji mikuu ya nchi zao.