Iran: Tumefanya mazungumzo mazuri na IAEA kuhusu nyuklia
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya Sheria na ya Kimataifa amesema kuwa, mazungumzo yake na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, Rafael Mariano Grossi, yalikuwa ya wazi na ya maana.
Kazem Gharibabadi ameandika hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kwa kusema: "Nimekuwa na mazungumzo ya wazi na yenye kujenga na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki."
Katika mazungumzo hayo, kumejadiliwa mambo mengi ukiwemo ushirikiano kati ya Iran na IAEA, utatuzi wa masuala mawili yaliyosalia, usalama wa vituo vya nyuklia na matukio mengine ya hivi karibuni yanayohusiana na mradi wa amani wa nyuklia wa Iran na kuondolewa vikwazo.
Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA ni pande mbili zenye historia ndefu ya ushirikiano unaoziwezesha kutatua tofauti chache zilizopo, mradi tu mashinikizo ya kisiasa ya nje ya wakala huo, yasiwepo. Kinachoharibu misimamo ya kugongana ya IAEA ni madola ya kibeberu kutouruhusu wakala huo kuchukua misimamo huru, ya kiutaalamu, isiyo na upendeleo na iliyoko mbali na mashinikizo ya kigeni.
Iran imejitolea kushirikiana na wakala wa IAEA ndani ya fremu ya kisheria ya majukumu ya wakala huo, sambamba na Tehran kulinda ussalama wake na maslahi yake ya kitaifa.
Jana Jumatatu asubuhi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei alitangaza kuwa, Gharibabadi ataelekea mjini Vienna kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA.