Araghchi: Maadui watajuta kwa kutoa vitisho dhidi ya Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitamruhusu mtu yeyote kuzungumza nayo kwa lugha ya ubabe na vitisho, akiwaonya maadui kwamba watajuta kulitishia taifa hili.
Katika mahojiano na Televisheni ya Al-Masirah ya Yemen, Araghchi amepuuza dhana kwamba mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen ni utangulizi wa uchokozi na uvamizi dhidi ya Iran.
Amebainisha kuwa, "Madai hayo si jambo geni kwa Iran, kwani vitisho hivyo vimesikika mara nyingi huko nyuma," na kuongeza kuwa, "Iran kamwe haitavumilia vitisho na haitaruhusu mtu yeyote kuzungumza kwa lugha ya vitisho. Maadui watajutia vitisho vyao."
Wakati huo huo, Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC ameonya kwamba, wanajeshi wa Marekani katika eneo hili wapo katika "nyumba ya vioo" na wanapaswa kuepuka "kuwarushia wengine mawe."
Hajizadeh amesema, "Wamarekani wana kambi 10 [za kijeshi] katika eneo, hasa karibu na Iran, na kwamba wanajeshi 50,000 waliomo (kwenye kambi hizo) wapo ndani ya shabaha ya Iran."
Iran hii leo inaadhimisha miaka 46 tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku taarifa rasmi zikisisitiza dhamira ya taifa hili na utayarifu wake wa kijeshi dhidi ya maadui, huku ikipuuzilia mbali vitisho vya Rais wa Marekani, Donald Trump vya "kuishambulia" nchi hii.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetoa taarifa kwa mnasaba wa siku hii na kusema, kukwea kwa Iran katika nafasi mashuhuri ya kieneo, pamoja na kuporomoka kwa madola ya kibeberu duniani, ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya kimataifa ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa IRGC, mahudhurio makubwa ya wananchi wa Iran katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yalitoa jibu thabiti kwa propaganda za adui zenye lengo la kulikatisha tamaa taifa la Iran.