Araghchi: Diplomasia ya Iran inazuiliwa na vitisho vya kivita vya Marekani
-
Sayyid Abbas Araqchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepuuzilia mbali mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani na kuyataja kuwa yasiyo na maana kutokana na vitisho vya Washington vya kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran.
Aidha ameeleza kuwa wazi Tehran kwa diplomasia na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja.
Abbas Araqchi aliyatoa maelezo hayo jana Jumamosi, siku mbili baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kudai kuwa Iran iko tayari kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja na utawala wake.
Trump amekuwa akitishia mara kwa mara kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran na alituma barua kwa nchi hiyo, ambayo amepata majibu yake.
Araqchi amesema kuwa maudhui ya barua ya Iran ilendana na ile ya Trump huku ikitoa nafasi ya kutumia diplomasia.
Ameongeza kuwa: “Kimsingi ni kuwa, mazungumzo ya moja kwa moja hayana maana ikiwa upande wa pili unatishia kutumia nguvu na kukiuka Mkataba wa UN, na maafisa wake wanaonyesha mitazamo inayokinzana."
Amesema: “Hata hivyo, tunaendelea kujitolea kwa diplomasia na tuko tayari kujaribu njia ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja.”
Araqchi pia amezungumzia kuhusu kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, yanayojulikana rasmi JCPOA, licha ya hatua za hiari za Iran kuhakikisha mpango wake ya nyuklia ni wa malengo ya amani.
Jamhuri ya Kiislamu, imesisitiza, sasa iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu shughuli zake za nyuklia kwa masharti ya kuondolewa vikwazo vikali kama hatua ya kujenga imani.
Araqchi pia amesema: “Wakati tukiendelea na njia ya diplomasia na mazungumzo ili kutatua sutafahamu na mifarakano, Iran inajiweka tayari kwa matukio yote yanayoweza kutokea."
Zaidi ya hayo, katika maelezo yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mataifa ili kukomesha mateso ya watu wa Palestina huku utawala haramu wa Israel ukiendeleza mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Gaza. Aidha ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kuzuia uvamizi utawala wa Israel dhidi ya Lebanon na Syria.