Iran yaadhimisha Siku ya Teknolojia ya Nyuklia kwa kuzindua bidhaa nane
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i124960-iran_yaadhimisha_siku_ya_teknolojia_ya_nyuklia_kwa_kuzindua_bidhaa_nane
Rais Masoud Pezeshkian ametembelea maonyesho ya mafanikio ya nyuklia huku Iran ikiadhimisha Siku yake ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia kwa kuzindua bidhaa nane.
(last modified 2025-04-09T09:03:57+00:00 )
Apr 09, 2025 09:03 UTC
  • Iran yaadhimisha Siku ya Teknolojia ya Nyuklia kwa kuzindua bidhaa nane

Rais Masoud Pezeshkian ametembelea maonyesho ya mafanikio ya nyuklia huku Iran ikiadhimisha Siku yake ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia kwa kuzindua bidhaa nane.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Mohammad Eslami, pamoja na kundi la maafisa waandamizi waliandamana na Rais Pezeshkian katika ziara yake katika shirika hilo mjini Tehran siku ya Jumatano.

Maonyesho hayo yanaonyesha mafanikio ya Iran katika mzunguko wa mafuta ya nyuklia, uzalishaji wa nishati na umeme, uzalishaji wa maji mazito na bidhaa zake, madawa ya nyuklia (radiopharmaceuticals), teknolojia ya plasma, matumizi ya mionzi, na teknolojia nyingine za kisasa zinazohusiana.

Maonyesho hayo yanajumuisha mabanda yanayoonyesha mafanikio ya ndani katika nyanja za jiografia ya anga kwa kutumia ndege (airborne geophysics), miradi ya uchunguzi na uendeshaji wa migodi ya urani, uzalishaji wa “keki ya njano,” usindikaji wa urani, utengenezaji wa vijisahani vya mafuta (pellets) na mitambo ya mafuta, pamoja na mchakato wa kurutubisha urani.

Sehemu moja ya maonyesho hayo imetengwa kwa ajili ya kuonesha miradi inayohusiana na mitambo ya umeme ya nyuklia, ikijumuisha maendeleo ya ujenzi wa Mitambo ya Bushehr Awamu za 2 na 3, ripoti ya kiwango cha uzalishaji umeme wa Kituo cha Bushehr Awamu ya 1, ambacho ni kituo cha kwanza cha nyuklia cha Iran, ripoti ya ujenzi wa Kituo cha Nyuklia cha Karoun, pamoja na usanifu na utengenezaji wa vipuri vinavyohitajika kwa ajili ya mtambo wa Bushehr.

Sehemu nyingine imejikita katika uzalishaji wa maji mazito na misombo ya deuteriamu, uzalishaji wa madawa ya nyuklia, vifaa vya vipimo vya nyuklia, maendeleo ya teknolojia ya plasma, matumizi ya mionzi katika tiba na kilimo, mionzi ya damu, utengenezaji wa viharakisha viwandani (industrial accelerators), na teknolojia mpya kama quantum na teknolojia za quantum.

Katika miaka ya hivi karibuni, wanasayansi wa Iran wamepiga hatua kubwa katika nyanja ya teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani licha ya vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi.

Hii ni mara ya 18 kwa Iran kuadhimisha siku ya kitaifa kuonesha mafanikio yake katika sekta ya nyuklia.