Pezeshkian: Iran katu haitaacha haki zake za nyuklia
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametangaza kwa msimamo thabiti kuwa Iran haitalegeza msimamo wala haitakubali masharti yoyote yanayohusu mafanikio yake ya nyuklia, huku akikosoa vikali vitisho vya kijeshi kutoka Marekani.
Akitangaza msimamo huo katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia na uzinduzi wa mafanikio mapya ya kiteknolojia katika sekta hiyo, Rais Pezeshkian alisisitiza kuwa kadri Marekani inavyoendelea kutoa vitisho, ndivyo Iran itakavyosimama imara zaidi.
Amesema kwa msisitizo. “Tunataka amani na usalama, na tuko tayari kwa mazungumzo – lakini kwa misingi ya heshima na kujivunia taifa letu. Hatutarudi nyuma kutoka kwenye mafanikio yetu, hatutakubaliana na masharti dhidi ya mafanikio hayo, na hatutamruhusu yeyote kutuzuia kufikiri, kubuni, wala kuwa na ubunifu,”
Rais huyo pia alieleza kwa mara nyingine kuwa Tehran haina dhamira ya kutengeneza bomu la nyuklia.
Aidha amesema: “Wamagharibi wanadai kuwa Iran inataka kutengeneza mabomu ya nyuklia. Ni nani mwenye mamlaka zaidi kuhusu suala hili kuliko Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatulah Sayyid Ali Khamenei, ambaye kwa uwazi kabisa na hadharani ametangaza kuwa hatutafuti kutengeneza bomu la nyuklia? Mmehakiki kauli hiyo mara mia, na mnaweza kuhakiki mara elfu nyingine zaidi, lakini fahamuni hili: tunahitaji sayansi ya nyuklia na nishati ya nyuklia katika kila sekta ya maisha."
Akitilia mkazo kuwa Iran haitafuti vita, Rais Pezeshkian alisema taifa hilo litaendelea kuwa thabiti dhidi ya aina yoyote ya uchokozi.
“Hatutafuti vita, lakini kwa maarifa na uwezo uliotengenezwa na watoto wetu, tutasimama imara mbele ya uvamizi wowote. Kadri wanavyotupiga, ndivyo tutakavyokuwa imara zaidi; kadri wanavyotutishia, ndivyo tutakavyokaza msimamo wetu. Sisi si wavamizi, wala hatuna nia ya kumshambulia yeyote,” alisema.
Aidha, aliashiria kauli za Ayatullah Khamenei kuwa Iran iko tayari kwa mazungumzo, lakini si kwa njia ya moja kwa moja, kwani taifa la Iran halina imani na upande wa pili.
Pezeshkian alihoji hivi: “Wanawezaje kutuwekea vikwazo vya rasilimali zetu na mawasiliano yetu, halafu watutake tuketi kwenye meza ya mazungumzo nao?”.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais Pezeshkian aligusia makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani (JCPOA), ambayo Marekani ilijitoa kinyume na makubaliano hayo mwaka 2018 na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, wakati huo Iran ikiwa bado inatimiza masharti yake kikamilifu.
Rais wa Iran ammebaini kuwa: “Sisi tulitimiza wajibu wetu chini ya JCPOA, lakini wao ndio waliokiuka makubaliano. Hatukutaka kujitoa. Walitupa vitisho kila siku. Na wanapotutisha, hatuna budi kujibu." Aidha Rais Pezeshkian amesema: “Nina hakika kuwa tutaweza kuendelea na njia yetu kwa nguvu, na kupitia mazungumzo yatakayofanyika, tutatatua changamoto hizi pia."
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, maafisa wa ngazi ya wa Iran na Marekani wamepangwa kukutana katika mji mkuu wa Oman, Muscat, siku ya Jumamosi, kwa ajili ya kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na suala la kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Tehran.