Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran: Israel haina uthubutu wa kutushambulia
(last modified Sun, 20 Apr 2025 02:55:08 GMT )
Apr 20, 2025 02:55 UTC
  • Sayyid Abbas Araghchi
    Sayyid Abbas Araghchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "si Israel pekee ambayo haina uthubutu wa kutushambulia, lakini hata Marekani pia haikubali kubahatisha kujiingiza kwenye chokochoko hatari kama hiyo."

Akizungumza alipokuwa ziarani nchini Russia, Sayyid Abbas Araghchi amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijarudi nyuma katika kuutetea hata mmoja kati ya misimamo yake ya haki na uadilifu na akaongeza kuwa, mashinikizo hayataifanya Iran iache kulinda heshima, sharafu na maslahi yake ya kitaifa.
 
Mkuu wa chombo cha diplomasia cha Iran amesisitiza kuwa, ni baidi kwamba vitisho vya kijeshi vinavyotolewa vitafikia hatua ya kutekelezwa, kwa sababu hata Wamarekani wenyewe wanaelewa kwamba Iran inafahamu vizuri jinsi ya kujilinda.
 
Araqchi amesema: "njia ya diplomasia iko wazi kwa Iran, lakini kama mazungumzo yatakabiliwa na hali ngumu na nzito, Iran imeshajiweka tayari kikamilifu kwa ajili ya njia nyinginezo".
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, Israel haijawahi wakati wowote huko nyuma kuwa na uwezo wa kuishambulia Iran, hainao hivi sasa, na haitakuwa nao katika siku zijazo. Na hata kwa kusaidiwa na Marekani, hawana uwezo wa kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya Iran.

Araghchi amesisitiza kuwa, Iran ina uwezo wa kujilinda hata dhidi ya Marekani na akaongezea kwa kusema, "Washington inafahamu Iran ina uwezo wa kiwango gani wa kujibu mapigo, na hata utawala wa Kizayuni pia unatambua vyema nguvu zetu za kiulinzi na uwezo wetu wa kujibu mapigo.../