Iran yawaonya maadui: Jeshi la Anga liko mstari wa mbele kujibu kitisho chochote haraka
(last modified Mon, 05 May 2025 12:11:19 GMT )
May 05, 2025 12:11 UTC
  • Iran yawaonya maadui: Jeshi la Anga liko mstari wa mbele kujibu kitisho chochote haraka

Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Brigedia Jenerali Hamid Vahedi amesema, kikosi hicho kiko mstari wa mbele kukabiliana haraka sana na tishio lolote dhidi ya nchi.

Vahedi ameyasema hayo, alipohutubia hadhara ya washiriki wa kozi ya 25 ya wasomi wenye vipawa wa vyuo vikuu.

Amesema: "Jeshi la Anga si kitengo cha vita tu katika mkakati wa ulinzi wa kitaifa, lakini pia liko mstari wa mbele katika kukabiliana haraka na kitisho chochote" .

Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Iran amebainisha kuwa "kudhibiti na kutawala anga kunamaanisha kutawala uwanja wa vita na kuhifadhi umoja wa ardhi yote", akaongeza kuwa katika milingano ya kijeshi ya leo taifa lisilo na uwezo wa kulinda anga yake litaendelea kuwa hatarini ardhini na baharini.

Aidha Jenerali Vahedi ametilia mkazo ustawi wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Iran katika miongo ya hivi karibuni na akasema: "leo, Jeshi la Anga linaweza kugundua vitisho kutoka maeneo ya mbali zaidi na kutoa jibu kali ndani ya muda mfupi kabisa".

Halikadhalika, Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa ndege erevu zisizo na rubanii, rada za safu-sawa, teknolojia ya vita vya kielektroniki (EW) na mifumo ya ulinzi wa anga ya matabaka kadhaa ni miongoni mwa zana zinazotumiwa na Jeshi la Anga la Iran kwa ajili ya kudumisha uwezo wake wa juu wa kiulinzi.../