Iran: Marekani inapotosha ukweli kuhusu urutubishaji wa urani
(last modified Sat, 10 May 2025 04:25:10 GMT )
May 10, 2025 04:25 UTC
  • Iran: Marekani inapotosha ukweli kuhusu urutubishaji wa urani

Behrouz Kamalvandi, msemaji na naibu mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), amepinga kauli za hivi karibuni zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kwamba ni nchi zenye silaha za nyuklia pekee zinazorutubisha madini ya urani yanayotumika kuzalisha umeme wa nyuklia.

Katika mahojiano ya televisheni wiki iliyopita, Rubio alidai, “Nchi pekee duniani zinazorutubisha urani ni zile zinazomiliki silaha za nyuklia.”

Alisema Iran “inapaswa kuachana na urutubishaji wa urani,” huku pia akidai kuwe na vikwazo dhidi ya mpango halali wa makombora wa Iran na kuruhusu wakaguzi wa Marekani kupata fursa ya kuingia katika vituo vyake vya nyuklia.

Akijibu kauli hizo, Kamalvandi amesema jana Ijumaa kwamba, “Iran si nchi pekee inayorutubisha urani bila kumiliki silaha za nyuklia. Ni changamoto kwa maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwamba waziri wao alitoa kauli kama hiyo bila kufanya utafiti sahihi.”

Kamalvandi ametaja nchi ambazo, kama Iran, zinarutubisha urani huku zikiwa zinapinga umiliki wa silaha za nyuklia.

“Nchi kama Ubelgiji, Uholanzi, Korea Kusini, Japan, Argentina, na Ujerumani zinasafisha urani na bado hazimiliki silaha za nyuklia,” amesema Kamalvani huku akiwataka maafisa wa Marekani kutoa “kauli za kwa makini” kuhusu masuala kama hayo.

Iran, ambayo imetia saini Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), inasisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani kabisa na uko ndani ya haki zake chini ya mkataba huo. Maafisa wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba usafishaji wa madini ya urani kwa madhumuni ya kiraia, kama vile mafuta kwa mitambo ya umeme wa nyuklia, unaruhusiwa chini ya sheria za kimataifa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Sayyid Ali Khamenei amepiga marufuku umiliki wa silaha za nyuklia katika Fatwa ambayo imetolewa kwa misingi ya kidini na maadili.

Rubio alitoa kauli hizo wakati wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, ambapo duru tatu tayari zimefanyika.