Vipaumbele muhimu zaidi vya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefafanua vipaumbele na masuala muhimu zaidi katika siasa za nje za Iran katika kikao cha Doha na pia katika vikao vingine na viongozi mbalimbali wa nchi za eneo.
Abbas Araghchi aliwasili Doha, Qatar kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa nne wa "Mazungumzo ya Iran na Nchi za Kiarabu." Katika hotuba yake katika mkutano huo, Araqhchi ameeleza na kufafanua masuala muhimu na vipaumbele vya siasa za nje za Iran.
Kabla ya kuelekea Doha, Araqhchi pia alikutana na kufanya mazungumzo na Faisal bin Farhan Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia ambapo wawili hao walijadili na kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande mbili na njia za kuimarisha uhusiano huo katika nyuga mbalimbali.
Kikao cha nne cha "Mkutano wa Mazungumzo ya Iran na Nchi za Kiarabu" kilifanyika Jumamosi, Mei 10, chini ya anwani ya "Mahusiano Madhubuti na Manufaa ya Pamoja" kwa ushirikiano na ushiriki wa Baraza la Kimkakati la Mahusiano ya Kigeni la Iran na Kituo cha Utafiti cha Al Jazeera.
Araqhchi pia alikutana na Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, huko Doha na kujadiliana naye masuala mbalimbali. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Qatar pia wamepitia matukio ya hivi karibuni ya kieneo hususan maafa ya kibinadamu huko Gaza kufuatia mauaji ya kimbari ya miaka miwili ya utawala wa Kizayuni na uzuiaji wake wa kupelekwa misaada ya chakula na matibabu katika ukanda huo na kusisitiza umuhimu wa kuwepo ushirikiano zaidi kati ya nchi za eneo ili kukomesha mateso yanayowakabili wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Duru mpya ya mashauriano ya Araqhchi na maafisa wa Qatar na Saudi Arabia imefanyika sanjari na duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, ambayo yanafanyika leo Jumapili, Mei 11, huko Muscat, mji mkuu wa Oman. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo yake nchini Qatar ameashiria mielekeo na vipaumbele muhimu zaidi vya siasa za nje za Iran.

Araqhchi amesema katika kikao cha Doha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeharamisha utengenezaji na matumizi ya silaha za nyuklia na kwamba daima imekuwa mwanachama anayewajibika wa kuzuia usambazaji wa silaha hizo. Pamoja na hayo, inasisitiza juu ya haki yake ya kutumia kwa amani nishati ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na haki ya kurutubisha madini ya urani.
Amesema: "Katika kipindi cha mwaka uliopita, tumeshuhudia matukio mengi machungu katika eneo la Asia Magharibi, lakini licha ya machungu hayo yote, matukio hayo yameleta pamoja mitazamo ya nchi za eneo na kuziwezesha kufikia maelewano ya pamoja mbele ya matukio na vitisho."
Huku akiashiria kuwa, lengo la utawala wa Kizayuni katika uvamizi wake huko Gaza ni kuharibu, kudhoofisha, kuua maelefu ya raia wa nchi za Kiislamu na kukalia kwa mabavu ardhi zaidi za nchi za eneo, Araghchi amesema: "Kukabiliana na maovu hayo ni wajibu wa kisheria na kimaadili wa serikali zote za eneo hili. Matukio haya yanapasa kufanya mjadala huu kuwa wa kuweka msingi wa kushajiisha ushirikiano badala ya siasa za kupimana nguvu."
Safari hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika eneo, inasisitiza ushirikiano zaidi wa nchi za eneo ili kuleta utulivu na maelewano kati ya majirani. Jinai za utawala ghasibu wa Israel zimezifanya nchi za Kiislamu kuhisi umuhimu wa kushirikiana kwa ajili ya kulinda haki za wananchi wa Palestina.
Katika upande wa pili, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia mkazo kuheshimiwa haki zake halali katika matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, na ndio maana katika mazungumzo yake yasiyo ya moja kwa moja na upande wa Marekani, ikawa inasisitiza umuhimu wa kutokiukwa mistari yake myekundu kuhusiana na suala hilo.
Kujenga uaminifu, utulivu, kupinga uingiliaji wa kigeni na umuhimu wa ushirikiano wa kieneo ni vipaumbele muhimu zaidi vya sera za kigeni za Iran katika mashirikiano yake na nchi za eneo. Matukio ya kisiasa na kijeshi katika eneo katika miezi ya hivi karibuni yameongeza umuhimu wa kuwepo maelewano zaidi baina ya majirani, jambo ambalo litakuwa na nafasi muhimu katika kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni.
Mtazamo wa kidiplomasia wa Iran katika siasa za nje katika miaka ya hivi karibuni daima umekuwa ni wa kupanua ushirikiano na majirani na nchi za Kiislamu, na makubaliano ya kieneo pia bila shaka yataimarisha uhusiano kati ya Iran na nchi za Kiarabu.