Wabunge wa Iran walaani hatua ya Bunge la UK kuitambua IRGC kuwa 'kundi la kigaidi'
Wabunge wa Iran wamelaani vikali hatua ya wabunge wa Bunge la Uingereza ya kuliorodhesha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuwa shirika la kigaidi, wakiapa kuchukua hatua za kisheria za kujibu mapigo.
Wakati wa kikao cha wazi cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) jana Jumanne, Ahmad Naderi, mjumbe wa bodi inayosimamia Bunge, alisoma taarifa kujibu hoja ya zaidi ya wajumbe 550 wa Bunge la Chini na Baraza la Juu la UK dhidi ya IRGC.
Taarifa hiyo imekashifu hatua ya wabunge wa Uingereza na kueleza kuwa ni "upumbavu na uadui," ikisisitiza kwamba Bunge la Iran, kwa kuzingatia wajibu wake wa kisheria wa kutetea mamlaka ya kitaifa, usalama na mamlaka ya Vikosi vya Wanajeshi wa Iran, linapinga vikali hatua hiyo ya Uingereza.
Imesema uamuzi huo wa UK, uliopasishwa kwa "amri ya utawala wa Kizayuni na propaganda za kundi la kigaidi [la MKO]," hauna msingi wowote wa kisheria au uhalali wa kisiasa. Wabunge hao pia wameikosoa Uingereza kwa kushupalia mtazamo wake wa kikoloni na uingiliaji dhidi ya mataifa huru.

Ikirejelea "historia ya giza" ya Uingereza kuingilia masuala ya ndani ya Iran, taarifa hiyo imebainisha kuwa, Uingereza imekuwa ikihatarisha usalama na ustawi wa watu wa Iran mara kwa mara kupitia uingiliaji wake na vitendo vyake vya uchokozi.
Wakati huo huo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imeeleza kwamba, Jeshi la SEPAH ni taasisi ya kiutawala iliyotokana na muktadha wa taifa la Iran na ina utambulisho rasmi na wa kisheria unaotokana na katiba ya Jamhuri ya Kiislamu, ambayo, pamoja na vipengele vingine vya jeshi, ina jukumu la kulinda usalama wa taifa na mipaka ya Iran, pamoja na kuchangia kwa usalama imara na utulivu katika eneo ili kukabiliana na ugaidi.