Je, Iran ilipata mafanikio gani ya kimkakati katika Vita vya Siku 12?
(last modified Sun, 29 Jun 2025 04:24:07 GMT )
Jun 29, 2025 04:24 UTC
  • Je, Iran ilipata mafanikio gani ya kimkakati katika Vita vya Siku 12?

Licha ya Vita vya siku 12 kati ya utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kusababisha hasara kubwa ya kimaada na isiyo ya kimaada, lakini pia vimekuwa na mafanikio ya kistratijia kwa Iran.

Moja ya mafanikio muhimu ni kwamba licha ya kipigo kikali cha awali, Iran iliweza kuamka na kujizatiti haraka kwa kadiri kwamba ilifanikiwa kutoa mapigo mazito kwa utawala vamizi wa Israel.

Mafanikio mengine muhimu ni kufunguliwa anga ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, kwa ajili ya kuruhusu makombora mazito ya Iran yapenye na kufanya uharibifu mkubwa dhidi ya taasisi za kijasusi na kijeshi za utawala wa Tel Aviv, licha ya kuwepo matabaka kadhaa ya mifumo ya ulinzi wa anga. Kwa hakika, ingawa mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran ulikuwa dhaifu wakati huo kutokana na vitendo vya uharibifu na usaliti uliofanywa na majasusi wa Mossad kwa ushirikiano wa wasaliti na vibaraka wa ndani ya Iran, lakini pia mfumo wa ulinzi wa anga wa utawala wa Kizayuni ulikuwa hatarini zaidi licha ya mifumo yake ya hali ya juu na uungaji mkono wa moja kwa moja kutoka Marekani na nchi nyingine za Ulaya. Haya ni mafanikio muhimu yaliyoonyesha kuwa madai kwamba jeshi la Kizayuni haliwezi kushindwa ni uwongo mtupu na ni matokeo ya simulizi za vyombo vya habari vya Magharibi. Mafanikio haya ni muhimu sana kwa sababu kabla ya vita hivyo, propaganda na uvumi mkubwa ulikuwa umeenezwa kote duniani na wapinzani wa ndani na maadui wa kigeni kuhusu uwezo mdogo wa kijeshi wa Iran, lakini katika vita hivyo vya siku 12 ilidhihirika wazi kuwa uwezo wa makombora wa Iran ulikuwa mkubwa na wa kuwashtua maadui.

Mafanikio ya tatu muhimu ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeuthibitishia ulimwengu uwezo wake usiopingika katika uga wa makombora katika operesheni zake za kijeshi. Onyesho hilo la uwezo wa makombora limethibitisha kuwa, nguvu kuu ya kijeshi katika eneo la Asia Magharibi ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa sababu imefanikiwa kujilinda na wakati huo huo kuuadhibu utawala wa Kizayuni uliojizatiti kwa silaha za kisasa kwa msaada wa nchi za Magharibi, bila ya kutegemea usaidizi wa nchi yoyote ya kigeni.

Kombora la Iran aina ya Sijjil

 

Katika kipindi chote cha maisha yake haramu katika eneo hili, utawala wa Kizayuni ulikuwa haujawahi kupata hasara na maafa makubwa kama uliyopata mara hii, katika vita vyovyote vile. Kuonyeshwa picha za uharibifu mkubwa uliofanyika katika miji yake muhimu kama vile Tel Aviv na Haifa, pamoja na kuthibitisha uwongo wa kuwepo usalama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, pia kumetilia shaka kubwa madai ya utawala huo kuhusu njia za usafiri na mipango ya kiuchumi.

Mafanikio mengine muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita vya siku 12 ni shambulio la pili la Iran dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika kipindi cha miaka 6 iliyopita. Shambulio la kwanza lilifanyika mnamo Januari 2020 dhidi ya kambi ya Marekani huko Ain al-Asad nchini Iraq, kufuatia mauaji ya Meja Jenerali Qassem Soleimani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sasa, shambulio la pili limefanyika baada la Marekani kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran, ambapo vikosi vya jeshi la Iran vimelenga kwa makombora kambi ya jeshi la anga la Marekani huko Al-Udeid nchini Qatar. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, hakuna nchi yoyote iliyothubutu kushambulia kituo chochote cha Marekani, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya shambulio hili kwa mara ya pili. Muhimu zaidi ni kwamba, mashambulio yote mawili yamefanyika wakati wa utawala wa Donald Trump mwenye madai na majigambo mengi. Kwa maneno mengine ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiogopi makelele na mayowe ya rais wa Marekani.

Mafanikio mengine muhimu ni kwamba propaganda zilizoenezwa na maadui wa mfumo wa Kiislamu kwamba wananchi hawaupendi mfumo huu zilibainika wazi kuwa ni porojo tupu, kwa sababu watu wa Iran kimsingi walisimama kwenye safu moja ya utambulisho wao wa kitaifa na Kiislamu, ambapo kupitia mshikamano huo wa kitaifa, waliunga mkono kikamilifu mashambulio ya jeshi lao dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na hata kulitaka litoe mapigo makali zaidi dhidi ya utawala huo wa kibaguzi.

Mambo tuliyotaja ni baadhi tu ya mafanikio iliyoyapa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita hivi vya kulazimishwa, na bila shaka kuna mambo mengine mengi muhimu yanayoweza kuzungumziwa

 katika uwanja huo.