Iran na nchi tisa zalaani vikwazo vya mataifa ya magharibi dhidi ya nchi zinazoendelea
Iran pamoja na nchi zingine tisa zimelaani vikali vikwazo vya upande mmoja na hatua za kulazimisha zinazowekwa na mataifa ya Magharibi dhidi ya nchi mbalimbali, wakizitaja kuwa ni ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni ya kutokujihusisha na mambo ya ndani ya mataifa mengine.
Katika tamko la pamoja lililotolewa Jumanne wakati wa kikao cha 53 cha Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), mataifa yaliyotia saini yalisisitiza umuhimu wa kuheshimiwa mamlaka kamili ya nchi, yakieleza kuwa vikwazo hivi vinapunguza uwezo wa mataifa, hasa yale yanayoendelea, kufikia malengo yao ya maendeleo endelevu.
Tamko hilo pia liligusia athari hasi za hatua hizi za kulazimisha katika sekta ya nishati ya kisukuku na mnyororo wa usambazaji wa viwanda muhimu kama vile vya chakula, kemikali na viwanda vizito.
Mataifa hayo tisa yameeleza wasiwasi wao mkubwa na kukataa kwao kwa nguvu hatua hizi za upande mmoja, yakizitaja kuwa ni batili, kinyume cha sheria za kimataifa, na ni ukiukaji wa wazi wa Hata ya Umoja wa Mataifa. Aidha, wameongeza kuwa hatua hizi ni uingiliaji wa moja kwa moja katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Tamko hilo limeeleza kuwa mienendo kama hii inadhoofisha misingi ya ushirikiano wa kimataifa na uamuzi wa pamoja (multilateralism), ambayo ndio nguzo kuu ya shughuli za Umoja wa Mataifa.
Mataifa haya yametoa wito kwa jamii ya kimataifa kupinga na kulaani vikwazo vya upande mmoja vinavyokiuka sheria za kimataifa, huku yakisisitiza haja ya hatua za kisheria na kiutawala kuchukuliwa ili kupunguza athari hasi za vikwazo hivyo katika nchi zisizohusika moja kwa moja.
Katika sehemu ya mwisho ya tamko hilo, nchi wanachama wa UNIDO zimetakiwa kulaani kwa nguvu hatua hizi zinazoleta madhara na zisitambue wala kuzitekeleza, zikisisitiza kuwa hatua madhubuti za kisheria zinahitajika kupambana na athari za vikwazo hivi vinavyojaribu kuingilia mamlaka ya mataifa mengine.
Tamko hilo limeidhinishwa na Iran, Belarus, China, Cuba, Korea Kaskazini, Nicaragua, Mamlaka ya Palestina, Russia, Sudan na Venezuela.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya kikatili kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya kwa sababu ya mpango wake wa nyuklia wa amani.
Vikwazo hivi vya upande mmoja vimekuwa kikwazo katika hatua kadhaa za maendeleo ya Iran, lakini kwa ujumla vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kujitegemea kwa taifa hili, na kuimarisha ari ya kitaifa ya kusukuma mbele mipaka ya ubunifu wake na kujitosa katika sayansi za kisasa za kiteknolojia bila kutegemea msaada wa mataifa ya kigeni.