IRGC yaonya Israel: Iran haitazingatia 'mistari miekundu' ikishambuliwa tena
-
Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema kwamba Iran haitazingatia tena 'mistari miekundu ya kijeshi au kisiasa endapo utawala wa Israel utafanya tena kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya al-Mayadeen siku ya Ijumaa na kuongeza kuwa: "Utawala wa Israel ulishindwa kufanikisha malengo yake wakati wa siku 12 za uchokozi wake dhidi ya Iran.
Majibu ya haraka ya Iran yalivuruga kabisa mahesabu ya maadui." Ameongeza kuwa: "Katika vita ya karibuni, lengo kuu la adui lilikuwa kuharibu uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu."
Msemaji huyo wa IRGC amebainisha kuwa adui ametangaza waziwazi kuwa vita hiyo dhidi ya Iran vilikuwa na nia ya kuilazimisha nchi ijisalimishe na kuisambaratisha.
Jenerali Naeini amesema adui aligeukia hatua za kijeshi baada ya kushindwa kufanikisha malengo yake kupitia mazungumzo, na kuongeza kuwa: “Maadui wa Iran hawana uelewa wa kutosha kuhusu Jamhuri ya Kiislamu.”
Amesisitiza kuwa adui wa Kizayuni alikuwa analenga makamanda wa kijeshi wa Iran na alinuia kuleta hali ya kutoeleweka nchini humo, “lakini tulijibu kwa haraka.”
Ameongeza kuwa: "Utawala wa Israel una wasiwasi mkubwa kuhusu jibu la "kuangamiza" la Iran iwapo wataanzisha tena vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu."
Katika vita vya siku 12, aliongeza, Iran ilivurumisha idadi kubwa ya makombora na droni kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), ambapo mengi yalilenga maeneo ya "kijeshi, kiusalama na kiuchumi."
Mnamo Juni 13, Israel ilianzisha uchokozi wa wazi na usio na sababu dhidi ya Iran, na kuwaua makamanda wengi wa ngazi ya juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na raia wa kawaida wakiwemo wanawake na watoto.
Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani pia iliungana na Israel na kushambulia maeneo matatu ya nyuklia ya Iran , hatua iliyokiuka Hati ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Katika kujibu hujuma hiyo, vikosi vya Iran vililenga maeneo ya kimkakati katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu pamoja na kituo cha kijeshi cha al-Udeid nchini Qatar, ambacho ni kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika eneo la Asia ya Magharibi.
Mnamo Juni 24, kupitia operesheni zake za kisasi zilizotekelezwa kwa dhidi ya utawala wa Israel na Marekani, Iran iliweza kuwalazimisha wavamizi kuomba kusitisha uchokozi huo haramu.