Baqaei: Iran inaunga mkono uhuru, mamlaka ya kujitawala Syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono uhuru na mamlaka ya kitaifa ya kujitawala Syria.
Akikosoa undumakuwili wa mataifa ya Magharibi juu ya suala la kile wanachokiita haki za binadamu na uchokozi wa Israel dhidi ya Syria, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, "Umoja wa Ulaya ulielezea uchokozi wa kijeshi wa wazi wa Israel kuwa ni 'kushadidisha hali ya taharuki katika ardhi ya Syria."
"Huu ni mfano wa wazi wa kupotosha ukweli na kuficha "ulaghai" chini ya kivuli cha diplomasia," ameelezea Baqaei na kuongeza kuwa, "Ikiwa na historia ya kujivunia ya kusimama dhidi ya uchokozi na mienendo haramu, Iran inapinga kwa uthabiti upendeleo na undumakuwili."
"Kama ada, tunasimama na wananchi wa Syria na kuunga mkono kwa sauti kubwa uhuru wa kitaifa na mamlaka ya kujitawala ardhi yote ya Syria," ameongeza Baqaei.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea na mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Syria kwa lengo la kuzusha mgogoro nchini humo.
Tel Aviv imekuwa ikitumia uungaji mkono wa Marekani hususan katika siku za hivi karibuni kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo yake maovu nchini Syria.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, kitendo cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutochukua hatua dhidi ya hatua za kivamizi za utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi za eneo hili ni hatari sana na sababu ya kushadidisha kiburi cha utawala huo ghasibu.