Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Pakistan wakutana kwa mazungumzo mjini Islamabad
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129090
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Seneta Mohammad Ishaq Dar katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo mjini Islamabad.
(last modified 2025-08-09T10:34:08+00:00 )
Aug 03, 2025 06:25 UTC
  • Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Pakistan wakutana kwa mazungumzo mjini Islamabad

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Seneta Mohammad Ishaq Dar katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo mjini Islamabad.

Idara ya Mahusiano ya Umma ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imetangaza kuwa: Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo mbili wamesisitiza juu ya dhamira ya nchi zao ya kuimarisha uhusiano, wakitilia mkazo kupanuliwa ushirikiano kwa ajili ya utulivu wa kieneo, biashara na ushirikiano wa kiuchumi.

Araghchi na Ishaq Dar wamejadili pia kuongezwa maelewano na maingiliano baina ya nchi mbili katika maeneo muhimu ya maslahi ya pande zote.

Mawaziri wa Mambo ya Nje, Viwanda na Madini, Barabara na Maendeleo ya Mijini, Ulinzi na Usaidizi wa Vikosi vya Wanajeshi ni miongoni mwa maafisa wa Iran walioandamana na Rais Masoud Pezeshkian katika ziara yake rasmi ya siku mbili nchini Pakistan.

Ziara hiyo iliyoanza jana Jumamosi ni hatua ya mabadiliko makubwa katika uhusiano wa muda mrefu wa Tehran na Islamabad. Ziara hiyo imefanyika wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zinakaribia kuadhimisha miaka 78 ya uhusiano wao wa kidiplomasia; uhusiano ambao ulianza kwa pande mbili kutambuana rasmi na ukiwa hadi sasa umepitia misukosuko na miteremko mingi.

Katika ziara hiyo, viongozi wa nchi mbili watafanya mazungumzo kwa lengo la kufafanua upya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kuimarisha maelewano katika nyanja za usalama na kisiasa. Kubadilishana mawazo juu ya matukio yanayojiri hivi sasa katika eneo, ikiwa ni pamoja na hali ya Ghaza, Asia Magharibi, na matokeo ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni, itakuwa pia sehemu ya ajenda za mazungumzo hayo. Aidha, kuandaa ratiba ya mkutano wa Kamisheni ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Pakistan utakaofanyika mjini Tehran ni ajenda nyingine ya mazungumzo kati ya pande mbili.

Ziara hii inakamilisha mkutano wa tano rasmi kufanywa na viongozi wa Iran na Pakistan katika kipindi cha mwaka mmoja sasa na inafanyika miezi miwili tu baada ya ziara ya pamoja ya Waziri Mkuu na Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Pakistan mjini Tehran. Mazungumzo yanayofanyika kwa njia ya simu kati ya Dk. Pezshkian na Shahbaz Sharif kwa kipindi cha miezi kadhaa sasa, hususan kwa kuzingatia mivutano ya hivi karibuni ya kijeshi katika eneo, yanaonyesha nia ya dhati ya pande zote mbili ya kuimarisha ushirikiano baina yao. Ziara hii itakuwa na umuhimu maalumu sio tu katika kalenda ya kidiplomasia ya Iran na Pakistan, lakini pia katika milingano ya kijiopolitiki ya eneo.../