Araqchi: Kufunga Mlango Bahari wa Hormuz si sera rasmi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130066-araqchi_kufunga_mlango_bahari_wa_hormuz_si_sera_rasmi_ya_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesisitiza kuwa suala la kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz si msimamo rasmi wa Iran, na kusisitiza kuwa sera ya Tehran ni kudumisha amani na utulivu katika Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Aug 27, 2025 10:57 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesisitiza kuwa suala la kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz si msimamo rasmi wa Iran, na kusisitiza kuwa sera ya Tehran ni kudumisha amani na utulivu katika Ghuba ya Uajemi.

"Sera ya Tehran iko wazi kikamilifu, kudumisha amani na utulivu katika njia muhimu ya baharini ya Ghuba ya Uajemi." Sayyid Abbas Araqchi ameeleza haya katika mahojiano na gazeti la  Asharq Al-Awsat akiwa katika ziara mjini Jeddah, Saudi Arabia, kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC. 

Ameongeza kuwa, Iran inazalisha na kuuza nje mafuta, na uchumi wake unategemea pakubwa mafuta. 

Araqchi amesisitiza kuwa matukio ya karibuni huko Gaza, Lebanon, Syria, na shambulio la Israel na Marekani dhidi ya Iran yamebainishia wazi ni nani haswa adui halisi wa eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amegusia matarajio ya mazungumzo ya nyuklia na kusema: Iran ipo tayari kwa ajili ya mazungumzo adilifu na ya haki kuhusu miradi yake ya nyuklia.

Amesema, Tehran hivi sasa inafanya majadiliano na madola matatu makubwa ya Ulaya yaani Ufaransa, Uingereza na Ujerumani pamoja na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ili kuanzisha mfumo mpya wa ushirikiano. 

Ameongeza kuwa Iran itaingia tu katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani iwapo Washington itatoa dhamana na hakikisho kwamba haitafanya mashambulizi ya kijeshi wakati mazungumzo yakiendelea.