Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yamesababisha Israel hasara ya mabilioni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130154-mashambulizi_ya_kulipiza_kisasi_ya_iran_yamesababisha_israel_hasara_ya_mabilioni
Maafisa wa utawala wa Israel wamethibitisha kuwa mashambulizi ya kisasi ya Iran dhidi ya taasisi za Israel wakati wa vita vya siku 12 yamesababisha hasara ya mabilioni ya shekel kwa utawala huo, huku zaidi ya madai 53,599 ya fidia yakiwasilishwa.
(last modified 2025-08-29T07:13:11+00:00 )
Aug 29, 2025 07:13 UTC
  • Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yamesababisha Israel hasara ya mabilioni

Maafisa wa utawala wa Israel wamethibitisha kuwa mashambulizi ya kisasi ya Iran dhidi ya taasisi za Israel wakati wa vita vya siku 12 yamesababisha hasara ya mabilioni ya shekel kwa utawala huo, huku zaidi ya madai 53,599 ya fidia yakiwasilishwa.

Gazeti la Ynet limenukuu Mamlaka ya Ushuru ya Israel ikisema kuwa kiwango cha uharibifu kilichosababishwa na mashambulizi ya Iran “kimefikia rekodi ya juu kabisa.”

Kwa mujibu wa maafisa wa Israel, madai 53,599 ya uharibifu wa moja kwa moja yaliwasilishwa ndani ya kipindi kifupi cha siku 12 za vita.

Hasara hizo zilijumuisha uharibifu mkubwa kwa Taasisi ya Sayansi ya Weizmann—yenye uhusiano wa karibu na shirika la ujasusi la Mossad—pamoja na kufungwa kwa muda mrefu kwa biashara nyingi.

Maafisa wameonya kuwa jumla ya hasara, ikiwemo uharibifu usio wa moja kwa moja kama vile kusitishwa kwa shughuli za kibiashara, ni kubwa zaidi. Hali hii inaonyesha gharama isiyokuwa ya kawaida ambayo Israel imelipa kutokana na uchokozi wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ushuru, Shay Aharonovich, amesema: “Uharibifu wa moja kwa moja unakadiriwa kuwa si chini ya shekel bilioni 4 (dola bilioni 1.1), na uharibifu usio wa moja kwa moja, ambao bado haujakadiriwa, unaweza kufikia mabilioni zaidi.”

Hadi sasa, Mfuko wa Fidia ya Ushuru wa Mali umetoa shekel bilioni 1.6 (dola milioni 430) kwa ajili ya fidia ya uharibifu wa moja kwa moja.

Mnamo Juni 13, Israel ilianzisha shambulizi la kichokozi dhidi ya Iran, hatua iliyochochea vita vya siku 12 ambavyo vilisababisha vifo vya watu wasiopungua 1,064 nchini Iran, wakiwemo makamanda wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida.

Marekani pia iliingia vitani kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran—kitendo kilichokiuka kwa kiwango kikubwa sheria za kimataifa.

Kama jibu, Jeshi la Iran lililenga ngome za kimkakati na kijeshi za Israel pamoja na kituo cha kijeshi cha al-Udeid kilichopo Qatar, kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika eneo la Asia Magharibi.