Araghchi aikosoa Ulaya kwa kufumbia macho uchokozi wa US, Israel dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130706-araghchi_aikosoa_ulaya_kwa_kufumbia_macho_uchokozi_wa_us_israel_dhidi_ya_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ameyajia juu mataifa matatu ya Ulaya kwa mtazamo wao wa "kutowajibika" mkabala wa uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na vitisho vyao vya kuhuisha maazimio yaliyobatilishwa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jambo ambalo anaamini litazidisha tu mivutano iliyopo.
(last modified 2025-09-12T07:11:59+00:00 )
Sep 12, 2025 07:11 UTC
  • Araghchi aikosoa Ulaya kwa kufumbia macho uchokozi wa US, Israel dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ameyajia juu mataifa matatu ya Ulaya kwa mtazamo wao wa "kutowajibika" mkabala wa uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na vitisho vyao vya kuhuisha maazimio yaliyobatilishwa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jambo ambalo anaamini litazidisha tu mivutano iliyopo.

Araghchi aliyasema hayo Alkhamisi usiku katika mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na kusisitiza dhamira ya Iran ya kulinda haki na maslahi ya watu wake kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezi wa Silaha za Nyuklia NPT.

Ameutaka Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wake kuchukua msimamo thabiti dhidi ya mashambulizi haramu dhidi ya vituo vya amani vya nyuklia vya Iran.

Akiashiria msimamo wa ushirikiano wa Iran katika kuamiliana na mashirika ya kimataifa, Araghchi ametaka kufanyika mazungumzo ya kujenga yenye lengo la kutimiza wajibu wa ulinzi wa Iran, hasa kwa kuzingatia uvamizi wa hivi karibuni dhidi ya miundombinu yake ya nyuklia.

Amesisitiza umuhimu wa mataifa ya Ulaya na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutambua na kuunga mkono juhudi hizo za kidiplomasia.

Waziri Araghchi pia amezungumzia mgogoro wa kibinadamu unaoendelea huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, akilaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel na kuyataja kuwa ni janga duniani. 

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesisitiza wajibu wa pamoja wa jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa, akiwemo Katibu Mkuu, wa kusitisha uchokozi huo na kushughulikia janga linaloshuhudiwa Gaza.

Kwa upande wake, Guterres ameashiria hatua zilizopigwa hivi karibuni katika mazungumzo ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, na kukariri ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kuunga mkono juhudi za kidiplomasia kuhusiana na suala la nyuklia la Iran.