Kamanda wa IRGC: Iran itajibu kwa ukali na nguvu zaidi uchokozi wa maadui
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Mohammad Pakpour amesisitiza kuwa, Jeshi la Iran limejiandaa kikamilifu kutoa jibu thabiti na kali kwa chockochoko tarajiwa za maadui.
Meja Jenerali Pakpour ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua vitengo vya wanamaji vya IRGC vilivyotumwa katika Ghuba ya Uajemi, kusini mwa Iran.
Wakati wa ziara yake hiyo ya ukaguzi, Meja Jenerali Pakpour, Kamanda Mkuu wa IRGC, ametathmini kiwango cha utayarifu wa vita vya vikosi vya operesheni vilivyoko kwenye Visiwa vya Ghuba ya Uajemi kuwa barabara.
Akihutubia vikosi vya wanamaji katika eneo hilo, Meja Jenerali Pakpour alisema kuwa "Kama vile vikosi vya jeshi viliupigisha magoti utawala wa Kizayuni na Marekani katika vita vya kutwishwa vya siku 12, ikiwa harakati yoyote itafanywa na maadui katika bahari na visiwa hivyo, vikosi vya Jeshi la Iran na Jeshi la IRGC vitajibu kwa nguvu zote."
Vile vile ametaja ari ya juu ya majeshi na imani kubwa katika maadili ya Kiislamu kuwa sababu kuu ya nguvu ya wanajeshi wa Iran ambayo inawatia hofu zaidi adui.
Wakati huo huo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeonya kwamba, kitendo chochote kipya cha uadui dhidi ya Iran kitakabiliwa na jibu kubwa zaidi.
IRGC ilisema hayo katika taarifa yake ya Alkhamisi, kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kujiri Operesheni ya Ahadi ya Kweli 2, shambulio la kisasi la makombora la Jeshi la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.