Rais Pezeshkian:Iran na Kazakhstan ziimarishe uhusiano ili kukabiliana na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i134206-rais_pezeshkian_iran_na_kazakhstan_ziimarishe_uhusiano_ili_kukabiliana_na_marekani
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa Iran na Kazakhstan zinapaswa kuimarisha uhusiano wa karibu ili kukabiliana na ubeberu Marekani.
(last modified 2025-12-12T03:04:30+00:00 )
Dec 12, 2025 03:04 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian wa Iran (kushoto) na mwenzake Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev
    Rais Masoud Pezeshkian wa Iran (kushoto) na mwenzake Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa Iran na Kazakhstan zinapaswa kuimarisha uhusiano wa karibu ili kukabiliana na ubeberu Marekani.

Akizungumza Alhamisi mjini Astana, akiwa ameongozana na ujumbe wa ngazi ya juu, Rais Pezeshkian alisema matokeo ya ziara hiyo ni “hatua kubwa na ya kuamua” katika kuimarisha mahusiano ya pande mbili.

Akiwa pamoja na mwenyeji wake, Rais Kassym-Jomart Tokayev, Rais Pezeshkian alisisitiza kuwa “Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zimekuwa zikilenga utambulisho na uhuru wa mataifa huru. Katika mazingira kama haya, ni muhimu kukuza uhusiano wa pamoja kwa umakini na hisia zaidi.”

Rais wa Iran ameonya kuhusu mazingira magumu ya kikanda na kuongezeka kwa mitazamo ya upande mmoja katika siasa za kimataifa.

Aliongeza kuwa mataifa hayo mawili yamefanikiwa kufikia ongezeko la asilimia 40 katika biashara baina yao, na yako tayari kutekeleza ramani ya njia inayolenga kuongeza thamani ya biashara hadi dola bilioni tatu.

Rais Pezeshkian alieleza matumaini kuwa Tehran na Astana zitatumia zaidi uwezo wa sekta binafsi katika kukuza ushirikiano.

Amesema  kuwa Tehran na Astana hushirikiana kwa karibu katika masuala mengi ya kikanda na kimataifa, na kwamba “mataifa haya mawili yamekuwa na ushirikiano mzuri katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, na pia yamefikia makubaliano muhimu.”

Katika ziara hiyo, Iran na Kazakhstan zimetia saini hati 14 za ushirikiano mjini Astana, hatua ambayo viongozi wa pande zote mbili wameitaja kuwa ishara muhimu ya kupanua uhusiano wao.

Baada ya ziara ya Kazakhstan, Rais Pezeshkian ameelekea Turkmenistan, ambako mkutano wa kimataifa kuhusu amani utafanyika ukiwahusisha viongozi kadhaa wa mataifa.

Balozi wa Iran nchini Urusi, Kazem Jalali, amesema kuwa marais wa Iran na Russia watakutana na kufanya mazungumzo wakati wa mkutano huo nchini Turkmenistan.