Spika Qalibaf: Daima tunafuatilia kupanua uhusiano na nchi za Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i134288-spika_qalibaf_daima_tunafuatilia_kupanua_uhusiano_na_nchi_za_afrika
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, daima taifa hili limekuwa likifuatilia kupanua ushirikiano na mataifa ya Kiafrika.
(last modified 2025-12-14T09:07:07+00:00 )
Dec 14, 2025 07:11 UTC
  • Spika Qalibaf: Daima tunafuatilia kupanua uhusiano na nchi za Afrika
    Spika Qalibaf: Daima tunafuatilia kupanua uhusiano na nchi za Afrika

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, daima taifa hili limekuwa likifuatilia kupanua ushirikiano na mataifa ya Kiafrika.

Mohamed Baqir Qalibaf amesema hayo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na  Spika wa Baraza la Wawakilishi la Ethiopia Tagesse Chafo na kusisitiza udharura wa kustawishwa zaidi uhusiano wa Tehran na Addis Ababa.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran na Spika wa Bunge la Ethiopia wametoa wito wa kutumia uwezo wa makubaliano ya BRICS kuendeleza ushirikiano wa kibiashara.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa siku za nyuma unapaswa kuainisha ramani ya mustakbali na kuongeza kuwa: "Hatua yoyote nzuri ambayo pande hizo mbili zinaweza kuchukua pamoja inahitaji kuanzishwa kwa balozi ili kustawisha uhusiano wa kisiasa kuwa ni utangulizi wa kustawisha uhusiano wa kibunge, kiuchumi na kiutamaduni."

Qalibaf amesema kuwa, mivutano katika Pembe ya Afrika, Afrika Kaskazini na Asia Magharibi ni sehemu ya mipango ya nchi za Magharibi na kuongeza: "Wanataka kuleta ukosefu wa usalama kwa nchi huru na za Kiislamu. Suala la usalama wa nchi na mataifa ni suala jumuishi na lenye mafungamano."

Kwa upande wake Tagesse Chafo Spika wa Baraza la Wawakilishi la Ethiopia  amesema katika mazungumzo yake na Spika Qalibaf kwamba, "Nchi hizo mbili zina mambo mengi yanayofanana; Iran ina ustaarabu wa kale na utamaduni tajiri, na Ethiopia pia ina sifa kama hizo. Leo hii, masuala kati ya nchi hizo mbili yanafuatiliwa kupitia balozi asiye mkaazi wa Ethiopia nchini Qatar, na tunajaribu kuhakikisha ofisi za kibalozi za nchi hizo mbili zinakuwa amilifu kuhusiana na suala hili."