Iran yalaani shambulio la “kikatili” dhidi ya hafla ya Kiyahudi nchini Australia
-
Iran yalaani shambulio la “kikatili” dhidi ya hafla ya Kiyahudi nchini Australia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulio la “kikatili” lililolenga hafla ya Kiyahudi mjini Sydney, Australia, shambulio ambalo limeua watu wasiopungua 12 na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa X siku ya Jumapili amesema: “Msimamo wa Iran ni wazi: tunalaani shambulio lolote la kikatili dhidi ya raia huko Sydney, Australia."
Amebaini kuwa: “Vitendo vya kigaidi na mauaji ya halaiki vinapaswa kulaaniwa popote vinapotokea, kwa kuwa ni kinyume cha sheria na ni uhalifu."
Kauli ya Baghaei imetolewa saa chache baada ya watu wawili wenye silaha kufyatua risasi katika hafla ya Kiyahudi katika jiji la Sydney.
Mamlaka za Australia zilisema polisi walimuua kwa risasi mshambuliaji mmoja, huku wa pili akikamatwa na kuripotiwa kuwa katika hali mahututi.
Watu wasiopungua 29 walithibitishwa kujeruhiwa, wakiwemo maafisa wawili wa polisi, kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi wa Jimbo la New South Wales, Mal Lanyon—ambalo ndilo jimbo linalojumuisha mji mkuu Sydney.
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, amelitaja tukio hilo kuwa “la kutisha na la kuhuzunisha,” akiongeza kuwa, “Hakuna nafasi kwa chuki, ukatili au ugaidi katika taifa letu.”
Alisema vyombo vya usalama vinaendelea kuwatambua wote waliohusika na shambulio hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, pia ameaani shambulio hilo kupitia mitandao ya kijamii, akilitaja kuwa “la kinyama” na kuonyesha mshikamano na jamii ya Kiyahudi.
Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, Australia imekuwa ikishuhudia hasira kubwa ya umma kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yanayotekelezwa na utawala wa Israel huko Gaza tangu Oktoba 2023.
Waandamanaji wamekuwa wakipaza sauti zao dhidi ya vifo vya raia, uharibifu wa makazi, na uhalifu wa kivita unaotekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza.
Ripoti za mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya ndani zinaonyesha kuwa hisia za umma zimezidi kuelekea kukerwa na janga la kibinadamu Gaza, huku waandamanaji wakitaka serikali ya Australia kulaani vitendo vya Israel na kusitisha mauzo ya silaha kwa Tel Aviv.