Spika: Iran inajiimarisha kijeshi sambamba na diplomasia
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad-Bagher Ghalibaf amesema Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia diplomasia sanjari na kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi na kijeshi ili iweze kukabiliana na maadui zake.
"Sote tunaamini kwamba, diplomasia na ulinzi ni pande mbili za sarafu moja, ambazo zinalandana kwa uratibu, kwa intelijensia ya hali ya juu, na kwa mujibu wa maagizo na maagizo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi," Ghalibaf amesema hayo katika kikao cha Bunge leo Jumatatu.
Ameongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi walihudhuria kikao hicho cha fargha cha Bunge mapema leo, ambapo masuala yanayohusiana na duru ya hivi karibuni ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yalijadiliwa. "Kiliikuwa kikao kizuri sana," Ghalibaf amesema.
Ujumbe wa Iran na Marekani, ukiongozwa na Araghchi na Mjumbe Maalum wa Marekani Steve Witkoff, ulianza tena mazungumzo ya nyuklia katika mji mkuu wa Oman, Muscat siku ya Ijumaa, miezi minane baada ya vita vya Israel dhidi ya Iran Juni mwaka uliopita.
Mazungumzo hayo yalikuja huku Marekani ikiwa imetuma vikosi vya anga na vya majini katika eneo hili, na kutishia kushambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu tena.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, Tehran haitaachana na diplomasia lakini iko tayari kukabiliana na kitendo chochote cha uchokozi.