Kamanda Naeini: Iran inadhibiti kikamilifu Lango Bahari la Hormuz
-
Kamanda Ali Muhammad Naeini
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Lango Bahari la Hormuz linadhibitiwa kikamilifu na Iran na kwamba uchokokozi wowote utakabiliwa na jibu kali.
Kamanda Ali Muhammad Naeini, msemaji wa jeshi la IRGC amesema hayo akitoa tathmini yake kuhusu mwenendo wa vita na kujibu maswali mbalimbali kuhusu madai ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel eti ya kushinda na kuangamiza uwezo wa kiulinzi wa Iran.
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kislamu amesisitiza kuwa, maadui wamekiri kuwa wameshindwa na wamekiri uhakika halisi wa Jamhuri ya Kiislamu; na sasa wanafikiria jinsi ya kuamiliana na Jamhuri ya Kiislamu na kuhitimisha vita. "Haya yote ni kwa mujibu nyaraka na ushahidi ingawa hayadhihirishwi waziwazi, na mijadala yao ya ndani pia ni katika utaratibu huu" amesema kamanda Naeini.
Ameongeza kusema: Lango Bahari la Hormuz linasimamiwa kikamilifu na vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na adui ambaye anadai kudhibiti eneo hili bahari na kuliangamiza jeshi letu la majini kama ana uthubutu basi ajaribu kutuma manowari zake karibu na ukanda huu.
Amesema meli zote ambazo zilikuwa katika eneo hilo zikipeperusha bendera mbalimbali lakini umiliki wake ukihusishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zimeshambuliwa. "Adui awali alikuwa akidai kuwa atadhibiti Lango Bahari la Hormuz, atasindikiza meli na kudhamini usalama wa kanda hii, nishati na mafuta iwapo vita vitatokea, hata hivyo ametoroka na kuondoka katika eneo hili," amesema Kamanda Ali Muhammad Naeini.