Jeshi la Iran lasema meli 25 zimepita katika Lango la Hormuz
-
Jeshi la IRGC
Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetangaza kuwa meli 25, zikiwemo meli za mafuta, meli za mizigo (kontena), na meli zingine kibiashara, zimevuka Lango la Bahari la Hormuz katika kipindi cha saa 24 zilizopita hadi kufikia jana, baada ya kupata idhini na chini ya uratibu wa kiusalama wa jeshi hilo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Jeshi la Majini la IRGC siku ya Jumamosi, meli hizo zimevuka njia hiyo muhimu ya maji baada ya kupewa idhini na kupatiwa ulinzi na jeshi hilo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa udhibiti wa kiusalama wa Lango la Hormuz unaendelea kwa nguvu kamili, licha ya hali ya kutokuwa na usalama iliyojitokeza kufuatia uchokozi wa “jeshi la kigaidi la Marekani” katika eneo hilo.
Iran ililifunga Lango la Hormuz dhidi ya maadui zake na washirika wao kufuatia uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi hii ulioanza Februari 28 na kuendelea kwa siku 40.
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la habari la Reuters, IRGC inachukua nafasi kuu katika mfumo mpya wa usafirishaji wa ngazi mbalimbali, ambao unatoa kipaumbele kwa meli zinazohusishwa na washirika kama vile China na Russia, huku meli nyingine zikilazimika kufuata makubaliano ya kiserikali au kulipa ada maalumu kabla ya kupita.
Ripoti hiyo imesema kuwa IRGC hupitia nyaraka za utambulisho zinazowasilishwa na mmiliki au mwendeshaji wa meli, na wakati wa mchakato huo, wanaweza kuhitaji kukagua meli husika kimwili.
Lengo la ukaguzi wa utambulisho ni kubaini iwapo meli ina uhusiano wowote na Marekani au utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizotumwa kwa wadau wa usafirishaji na Mamlaka ya Lango la Ghuba ya Uajemi ya Iran, IRGC inawataka wamiliki wa meli kufichua taarifa ikiwemo thamani ya mzigo wa meli, bendera, mahali ilipotoka na inakoenda, mmiliki na msimamizi aliyesajiliwa, pamoja na utaifa wa mabaharia.
Makubaliano ya nchi mbili kwa ajili ya kupita yanajumuisha hatua ya ziada: Nchi husika huwasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ili kuomba idhini. Waziri huwasilisha maombi hayo kwa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.
Uamuzi hufanywa na kuwasilishwa kwa vyombo husika, ikiwemo IRGC, ambayo baadaye hutoa taarifa za kijiografia (coordinates) na maelekezo yanayohitajika kwa ajili ya safari salama.
Nchi nyingine zimefikia makubaliano tofauti. Miongoni mwao ni India, ambayo huagiza takriban 90% ya mahitaji yake ya mafuta na karibu 50% ya gesi, ambayo sehemu kubwa hupitia Hormuz.
Kulingana na afisa wa wizara ya usafirishaji ya India aliyenukuliwa na Reuters, New Delhi inatumia ubalozi wake mjini Tehran kuwasiliana na mamlaka za Iran kuhusu ukaguzii wa meli ambazo India inataka ziondoke katika Ghuba ya Uajemi.