Iran: Hatuna mipaka katika kuimarisha uhusiano wetu na Afrika
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haina mipaka katika kuimarisha uhusiano wake na bara la Afrika ikiwemo Algeria.
Es’haq Jahangiri amesema hayo leo hapa Tehran wakati alipoonana na Waziri wa Nishati wa Algeria Noureddine Bouterfa aliyeko ziarani hapa nchini Iran.
Bw. Jahangiri aidha amesema, baada ya kuondolewa vikwazo kufuatia makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1, sasa Iran inapigania kuimarisha uhusiano wake na nchi mbalimbali hususan na nchi rafiki kama Algeria.
Vile vile amesema, viongozi wa Iran wana nia ya kweli ya kuimarisha uhusiano wao na Algeria katika sekta zote na kusisitiza kuwa, kutembeleana viongozi wa nchi hizi mbili ni hatua nzuri ambayo itakuwa na athari za moja kwa moja katika jambo hilo.
Tarehe 16 Januari mwaka huu, Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumaini, zilianza utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA ambayo yalitiwa saini tarehe 14 Julai, 2015.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Iran ilikubali kuwekea mipaka fulani miradi yake ya nyuklia na upande wa pili nao ukaahidi kuondoa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyowekewa Iran kutokana na miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Algeria amesema kuwa, Tehran na Algiers zina misimamo mengi inayofanana hasa katika shirika la OPEC na ametoa mwito wa kupanuliwa wigo wa ushirikiano wa nchi hizo ndugu katika nyuga zote hususan za nishati.