Rais Rouhani asisitiza kuongezwa kiwango cha ushirikiano kati ya Iran na Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i16054-rais_rouhani_asisitiza_kuongezwa_kiwango_cha_ushirikiano_kati_ya_iran_na_kenya
Rais Hassan Rouhani amesema kustawisha na kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ni miongoni mwa misingi ya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 25, 2016 13:04 UTC
  • Rais Rouhani asisitiza kuongezwa kiwango cha ushirikiano kati ya Iran na Kenya

Rais Hassan Rouhani amesema kustawisha na kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ni miongoni mwa misingi ya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ameyasema hayo leo katika mazungumzo na Spika wa Bunge la Kenya Justin Muturi aliyeko safarini hapa nchini.

Rais Rouhani amesema, Kenya ni miongoni mwa nchi rafiki za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran barani Afrika; na Tehran inakaribisha kuinua kiwango cha ushrikiano wake na Nairobi hususan katika sekta ya uchumi.

Rouhani ameashiria uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sekta za utoaji huduma za kiufundi na uhandisi, ambapo sambamba na kueleza utayari wa Tehran wa kutekeleza miradi ya Kenya inayohusiana na kawi, ujenzi wa barabara, ujenzi wa mabwawa na sekta za nishati ameeleza kwamba: Kwa kuandaa suhula zinazohitajika, serikali ya Kenya inaweza kufungua njia zaidi ya kuandaa mazingira kwa ajili ushiriki na uwekezaji wa mashrika ya sekta binafsi ya Iran nchini humo.

Ujumbe wa Kenya ulipoonana na Rais Rouhani

Amesisitiza kuwa mazingira ya baada ya makubaliano ya nyuklia na kuondolewa vikwazo yameandaa mazingira ya kustawishwa zaidi ushirikiano baina ya nchi mbili.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Kenya Justin Muturi amesisitiza kuwa nchi yake imedhamiria kwa dhati kuinua na kustawisha kiwango cha ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga zote na kwamba kutekelezwa makubaliano ya nyuklia kumeandaa mazingira mazuri zaidi juu ya suala hilo.../