Iran na Thailand kuimarisha uhusiano wa pande zote
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nchi mbili za Iran na Thailand zina nia ya kweli ya kuimarisha uhusiano wao katika nyuga za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kielimu.
Rais Rouhani amesema hayo leo (Jumapili) katika kikao cha pamoja cha wajumbe wa ngazi za juu wa Iran na Thailand mjini Bangkok na kuongeza kuwa, Thailand ni daraja la kuweza Iran kulitumia kwa ajili ya kuingia na kujiimarisha kiuchumi katika eneo la mashariki mwa Asia.
Amesema, Iran nayo ina miundombinu bora kabisa katika nyuga tofauti kama bandari na suala zima la usafiri na uchukuzi, hivyo ni daraja bora la kuunganisha maeneo ya kusini na mashariki mwa dunia. Amesema, Iran ni nchi yenye usalama zaidi katika eneo hili na ni lango zuri zaidi la kuimarisha uhusiano wa kichumi baina ya mashariki mwa Asia, Asia ya Kati na Kafkaz.
Rais Rouhani aidha amesema, Iran haioni kizuizi chochote cha kuimarishwa uhusiano wake na Thailand katika nyuga zote na kwamba makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA, yanatoa fursa nzuri kwa nchi hizi mbili kuondoa mipaka yote katika kuimarisha uhusiano wao.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Thailand, Prayut Chan-o-cha, amesisitiza kuwa nchi yake ina nia ya kweli ya kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja zote na kuongeza kwamba, Iran inaweza kuwa kiungo kizuri sana cha kuiunganisha Thailand na maeneo ya katikati na magharibi mwa bara la Asia pamoja na bara Ulaya.