Iran kurusha satalaiti tatu anga za mbali
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepanga kutuma satalaiti zingine tatu katika anga za mbali katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Iran Mahmoud Vaezi amesema satalaiti hizo tatu ambazo zitarushwa katika anga za mbali zimetegenezwa na wanasayansi vijana Wairani katika vyuo vikuu nchini.
Amesema moja ya satalaiti hizo inajulikana kama Sharif Sat na itakuwa na jukumu la kufanya upelelekezi katika anga za mbali. Hali kadhalika amesema Iran hivi sasa iko katika mkakati wa kutengeneza satalaiti za mawasiliano na kwamba inapanga kushirikiana na nchi kadhaa katika mradi huo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeingia katika kundi la nchi 10 bora duniani katika sekta ya teknolojia ya anga za mbali.
Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa ijulikanayo kwa jina la Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009. Iran pia imetangaza kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanaadamu katika anga za mbali. Tayari mazoezi yameshafanyika kuhusiana na lengo hilo kwa kutumwa nyani hai katika anga za mbali ambaye alirejea ardhini akiwa salama. Mafanikio haya ya Iran yanajiri pamoja na kuwepo vikwazo vya kila upande vya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kislamu.