Araqchi: Marekani na baadhi ya nchi zimekuwa zikikwamisha utekelezwaji wa JCPOA
(last modified Sun, 15 Jan 2017 14:32:55 GMT )
Jan 15, 2017 14:32 UTC

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Tehran imekuwa ikikabiliwa na ukiukwaji wa ahadi, kigugumizi, siasa za ucheleweshaji mambo na chuki za Marekani na baadhi ya nchi katika utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Sayyid Abbas Araqchi  amesema hayo leo kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kubainisha kwamba, Wamarekani na madola ya Ulaya yalifanya kadiri yalivyoweza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ili kuweka vizingiti katika njia ya utekelezwaji wa makubaliano hayo ya nyuklia. 

Sayyid Abbas Araqchi

Amesema kuwa, hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya kadiri ya uwezo wake kukabiliana na vizingiti hivyo. Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitambulisha miradi ya nyuklia ya Iran kwa walimwengu kuwa ni halali na kubainisha kwamba, miradi ya nyuklia ya Iran itaendelea kwa nguvu zote kama kawaida na wakati huo huo uhakiki na ustawi wa miradi hiyo pia umo katika hali ya kufanyika.

Kuhusiana na vipengee vya mazungumzo ya hivi karibuni ya Iran na ujumbe wa Marekani huko Vienna Austria, Sayyid Abbas Araqchi amesisitiza kuwa, ukiachilia mbali masuala ya kiufundi katika suala la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) pamopja na mustakabali wake, Iran haina mazungumzo mengine na Marekani. 

Tags