Uturuki yaomba msaada wa Iran kumaliza vita katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i2491-uturuki_yaomba_msaada_wa_iran_kumaliza_vita_katika_eneo
Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema Tehran na Ankara zinapaswa kuwa na ‘msimamo wa pamoja’ ili kumaliza migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 05, 2016 13:51 UTC
  • Uturuki yaomba msaada wa Iran kumaliza vita katika eneo

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema Tehran na Ankara zinapaswa kuwa na ‘msimamo wa pamoja’ ili kumaliza migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati.

Davutoglu ameyasema hayo Jumamosi ya leo baada ya kuwasili hapa mjini Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi. Ameshiriki kikao cha pamoja na waandishi habari akiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Es’haq Jahangiri na kusema: “Ni muhimu kwa Uturuki na Iran kuwa na msimamo wa pamoja ili kumaliza mapigano kati ya ndugu katika eneo hili. "Tunapoaswa kumaliza malumbano ya kikabila na kimadhehebu,” amesema Waziri Mkuu wa Uturuki.

Aliongeza kuwa Tehran na Ankara zinahitilafiana katika baadhi ya masuala, “lakini hatuwezi kubadilisha historia au jografia yetu.”

Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema kurejeshwa amani Mashariki ya Kati kuna maslahi kwa Iran na Uturuki.

Ameongeza kuwa nchi mbili zina azma ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili hasa wa kibiashara. Amesema pande mbili zimeafikiana kuwa kiwango cha biashara baina ya nchi mbili kifike dola bilioni 30 kwa mwaka na kwamba mwezi ujao kutafanyika kikao cha pamoja kuondoa vizingiti vya kibiashara.