Dehqan: Juhudi za Israel za kuunda muungano dhidi ya Iran zitafeli
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema juhudi za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuunda muungano dhidi ya Iran hazitafua dafu.
Brigedia Jenerali Hussein Dehqan, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, jitihada hizo za utawala haramu wa Israel zilizochochewa na msimamo wa Iran wa kuiunga mkono Palestina, zitagoga mwamba.
Kauli ya Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni radiamali kwa matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel, Avigdor Lieberman na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence dhidi ya Iran.
Wakizungumza katika nyakati tofauti katika Kongamano la Kimataifa la Usalama la Munich nchini Ujerumani hivi karibuni, wawili hao walidai kuwa Iran inaunga mkono ugaidi na eti ndio nchi inayotishia zaidi usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Brigedia Jenerali Hussein Dehqan amesema eneo hili na dunia kwa ujumla haiwezi kusahau na kufumbia macho jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina kwa zaidi ya miaka 60 sasa na kuongeza kwamba maghala ya silaha za nyuklia ya utawala haramu wa Israel ndilo tishio kubwa zaidi kwa amani na usalama wa dunia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi, hivi karibuni alisema muungano na misimamo ya aina moja dhidi ya Iran iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Waziri wa Vita wa utawala ghasibu wa Israel na mwenzao wa Uturuki katika Mkutano wa Usalama wa Munich si jambo jipya wala lililotokea kwa sadfa na kubainisha kuwa, tawala hizo zinadhani kuwa, ili kuweza kufidia kufeli na kushindwa kwao mara kwa mara katika Mashariki ya Kati zinapaswa kuchochea anga ya kimataifa dhidi ya Iran.