Feb 22, 2017 16:52 UTC
  • Rais Hassan Rouhani akiwa katika mazungumzo na Spika wa Bunge la Uganda, Bi Rebecca Kadaga.
    Rais Hassan Rouhani akiwa katika mazungumzo na Spika wa Bunge la Uganda, Bi Rebecca Kadaga.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonana na maspika wa nchi kadhaa pambizoni mwa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina hapa mjini Tehran.

Miongoni mwa maspika walioonana na Rais Hassan Rouhani leo ni kutoka Palestina, Uganda, Jordan, Malaysia, Lebanon na Syria.

Katika mazungumzo yake na Bw. Salim al Zanoon, Spika wa Bunge la Palestina, Rais Rouhani amesema, Iran inalihesabu suala la Palestina kuwa ndilo suala muhimu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu na haizembei kuchukua hatua yoyote ile katika kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina. 

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Palestina ametoa ripoti kuhusiana na hali waliyo nayo hivi sasa Wapalestina hasa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza na kusema, haipasi kuruhusu jambo lolote lile lifunike kadhia ya Palestina na mapambano dhidi ya jinai za utawala pandikizi wa Israel.

Rais Rouhani katika mazungumzo na Nabih Beri, Spika wa Bunge la Lebanon

 

Rais Rouhani ameonana pia na Bi Rebecca Kadaga, Spika wa Bunge la Uganda na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya njama za kila namna za kujaribu kulisahaulisha suala la Palestina. Amesisitiza kuwa, nchi zote duniani zinapaswa kutangaza uungaji mkono wao kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina hususan kwa kuzingatia hali ilivyo hivi sasa kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake, Bi Rebecca Kadaga amepongeza hatua ya kufanyika kwa mafanikio mkutano huo wa kimataifa wa kuunga mkono mapambano ya Wapalestina na kusema, suala la Palestina ni suala la kimsingi na muhimu kwa nchi zote za Kiislamu.

Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina uliofanyika kwa muda wa siku mbili, umemalizika leo hapa mjini Tehran. 

Tags