Mar 17, 2017 03:59 UTC
  • Sheikh Ali Muhammadi, Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
    Sheikh Ali Muhammadi, Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Mkuu wa Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, siasa kuu za Tehran ni kupigania umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Ali Muhammadi akisema hayo jana na kuongeza kuwa, kinyume kabisa na propaganda za uongo na zenye malengo maalumu zinazotolewa na maadui wa umma wa Kiislamu, wakati wote Iran imeonesha kivitendo jinsi inavyopigania umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ameongeza kuwa, Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na viongozi wote wa Iran ni walinganiaji wakubwa wa umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu bila ya kujali madhehebu wala utaifa wa Waislamu hao.

 

Mkuu wa Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri ya Iran amesisitiza kuwa, taasisi yake ni moja ya vyombo vyenye jukumu la kufuatilia masuala ya kiutamaduni katika nchi za Kiislamu na daima inaendesha siasa zake kwa kuzingatia umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu.

Aidha amesema, magenge ya kigaidi kama vile Daesh, si wawakilishi wa Waislamu wa Kisuni na ndio maana wanavyuoni wakubwa wa Kisuni wametangaza bayana kwamba wako mbali na jinai zinazotendwa na magenge kama hayo.

Vile vile amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono harakati na fikra za muqawama bila ya kujali wanaoendesha harakati hizo ni Waislamu wa Kishia au Kisuni na huo ndio msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu tangu ilipoasisiwa.

Tags