Qassemi: Udiplomasia wa Saudi Arabia umewasha moto wa machafuko
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu matamashi yaliyotolewa na mwana mfalme ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia huko Marekani dhidi ya Iran akisema kuwa udiplomasia wa njozi na uliojaa uwongo wa viongozi wa Saudia umeshadidisha moto wa machafuko na ukosefu wa amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mohammad bin Salman Al Saud, naibu mrithi wa kiti cha ufalme ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia amedai asubuhi ya leo katika mazungumzo yake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis huko Washington kuwa, eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla inakabiliwa na hatari kutokana na hatua ya Iran ya kuwaunga mkono magaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi amesema kuwa katika miaka hii ambapo eneo la Mashariki ya Kati linakabiliwa na machafuko, Saudi Arabia si tu kuwa haijatoa msaada wowote ili kurejesha amani na utulivu, bali imezidisha hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani katika eneo hili kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi huko Syria na kuanzisha vita vikubwa dhidi ya watu wa Yemen.
Qassemi ameongeza kuwa udiplomasia wa njozi na uliojaa madai ya uwongo wa viongozi wa Saudia umemfanya Mohammad bin Salman ajigambe kuwa yeye ni mmoja wa waendeshaji wakuu wa vita vya Saudi Arabia dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen na mauaji na ukatili unaoshuhudiwa huko Syria, Bahrain na katika nchi nyingine za Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla.