Rouhani: JCPOA imetekelezwa kwa mujibu wa miongozo ya Kiongozi Muadhamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28462-rouhani_jcpoa_imetekelezwa_kwa_mujibu_wa_miongozo_ya_kiongozi_muadhamu
Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza makubaliano ya nyuklia ya Vienna kwa mujibu wa miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 30, 2017 16:13 UTC
  • Rouhani: JCPOA imetekelezwa kwa mujibu wa miongozo ya Kiongozi Muadhamu

Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza makubaliano ya nyuklia ya Vienna kwa mujibu wa miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Akihutubia umati wa watu katika mji bandari wa Bandar Abbas mkoani Hormozgan kusini mwa Iran, Rais Rouhani ameziasa pande zote kuhusika kuheshimu na kutekelezwa ipasavyo makubaliano hayo yanayofahamika kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Dakta Rouhani amesema, wakosoaji wa makubaliano hayo ya kihistoria wanapaswa kufahamu kuwa, JCPOA ni mafanikio kwa taifa zima la Iran na kusisitiza kwamba, makubaliano hayo ni mradi wa kitaifa.

Ikumbukwe kuwa, tarehe 14 Julai 2015, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani zilisaini mkataba kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran ambao utekelezaji wake ulianza Januari 16 mwaka uliopita wa 2016.

Askari wa SEPAH

Kwengineko katika hotuba yake, Rais Hassan Rouhani amepongeza nafasi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kuzidhaminia ulinzi na usalama nchi jirani.

Amesema: "SEPAH na Mapinduzi ya Kiislamu vimekuwa na taathira chanya katika kuwaunga mkono wananchi madhulumu kwenye nchi za Kiislamu kama vile Iraq, Syria na Lebanon."

Rais wa Iran ameongeza kuwa, kama si mchango muhimu na mkubwa wa Iran, magenge ya kigaidi yangelikuwa yamevuruga kikamilifu usalama na amani ya eneo hili na kusababisha matatizo makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na kote duniani.