Iran yataka ushirikiano baina ya nchi za Ghuba ya Uajemi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ametoa wito wa kuwepo urafiki miongoni mwa nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi.
Katika ujumbe aliotuma Jumapili katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Zarif amesema nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi zina uwezo wa kujiendeshea mambo yao kwa uhuru pasina kuwepo uingiliaji wa madola ajinabi.
Katika ujumbe huo alioutuma kwa munasaba wa Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi, Zarif alisema: "Kupitia ushirikiano, nchi za Ghuba ya Uajemi zinaweza kulinda maslahi yao na kujihami mbele ya vitisho." Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nchi za Ghuba ya Uajemi zinaendelea kukumbwa na tatizo la uingiliaji wa madola makubwa ambayo yamekuwa na nafasi haribifu ya kuibua vita na migogoro katika eneo.
Aidha Zarif amesema sera za kistratijia za Iran zimejengeka katika msingi wa kuwepo mazungumzo na ushirikiano wa pamoja na nchi jirani ili kutatua migogoro ya kieneo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kuandika katika sehemu nyingine ya ujumbe huo kuwa: "Sisi wakazi wa pande zote mbili za Ghuba ya Uajemi, pamoja na kuwepo baadhi ya hitilafu, tunaweza kuibadilisha bahari hii kuwa ya urafiki."
Tarehe 10 Ordebehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani sawa na tarehe 30 Aprili, inafahamika humu nchini kuwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi.
Siku hii iliitwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuiita Ghuba ya Uajemi kwa majina mengine bandia. Jina la kale na kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars.